10.8 C
New York

Serengeti ni Tunu ya Taifa na Urithi wa Dunia itunzeni

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini-Serengeti

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi kushirikiana kwa karibu na wahifadhi katika kulinda, kutunza na kuhifadhi maeneo yaliyotangazwa kama urithi wa dunia, yakiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa kuwa yana mchango mkubwa katika kutangaza taifa kimataifa, kuongeza watalii na kukuza pato la Taifa.

Akizungumza mjini Mugumu, wilayani Serengeti, jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia, Kanali Mtambi ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema ni muhimu jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali hizo adhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akitumia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Majanga na Migogoro ni Tishio kwa Urithi wa Dunia”, Mtambi alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya jamii na wahifadhi ndiyo njia bora ya kuhakikisha urithi huo unaendelea kudumu.

“Serengeti ni tunu ya taifa. Ninawapongeza wananchi wanaozunguka hifadhi hii kwa juhudi zenu. Agizo langu la kufanya vikao vya pamoja kila mwezi kati ya wananchi na wahifadhi limeleta mafanikio makubwa, na hali ya utunzaji imeimarika,” alisema.

Alitaja vituo saba vilivyotambuliwa kama urithi wa dunia na UNESCO kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Maeneo ya michoro ya miamba ya Kondoa, Pori la Akiba la Selous, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa UNESCO nchini, Anna Joyce Kalumuna, alisema mkataba wa UNESCO wa mwaka 1972 ambao Tanzania iliridhia mwaka 2005, umechangia kwa kiasi kikubwa kulinda maeneo hayo na kuongeza faida za kiuchumi na kitaaluma kwa nchi.

“Maeneo haya yanatangazwa kimataifa bila gharama kupitia machapisho ya UNESCO. Hii huongeza idadi ya watalii na kukuza utalii unaozingatia mazingira na tamaduni za jamii zetu,” alisema Kalumuna.

Awali, Zuberi Mabiye kutoka Idara ya Mambo ya Kale na Asha Ally kutoka Mji Mkongwe wa Zanzibar, waliwataka wananchi kuendeleza ushirikiano na wahifadhi ili kulinda urithi wa dunia kwa manufaa ya wote.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, aliwapongeza wahifadhi kwa kazi yao nzuri na kuwaomba wananchi kuwapa ushirikiano wa karibu ili hifadhi iendelee kuwa kivutio kikubwa cha watalii duniani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img