15.6 C
New York

Kwa nini Urusi haiingilii kati kuisaidia Iran dhidi ya Marekani, Israel?

Published:

TEHRAN, Iran

SAA chache baada ya Iran kuanza kushambuliwa makombora ya Marekani na Israel, Serikali ya Urusi ilitoa tamko zito.

Mwakilishi wa Urusi ndani ya Umoja wa Mataifa (UN), Vassily Nebenzia, alilaani mashambulizi hayo akiyaita kuwa ni ubabe wa Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Hata hivyo, tofauti na ilivyotarajiwa, kwamba Urusi ingeingia vitani kuisaidia Iran kupambana na mataifa hayo, hilo halijatokea.

Kwa miaka mingi, Urusi na Iran zimekuwa na uhusiano mzuri katika miradi ya kiuchumi, kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa za Mashariki ya Kati raia wa Azerbaijan, Nikita Smagin.

Kwa upande wake, Julian Waller, ambaye ni mtaalamu wa tafiti wa Taasisi ya CNA ya Marekani, anasema:

“Pia, Iran imekuwa na umuhimu mkubwa katika jeshi la Urusi, ambapo imekuwa ikiipatia ndege zisizo na rubani aina ya Shahed tangu mwaka 2023. Ndege hizo zimeisaidia sana Urusi katika vita yake na Ukraine.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi, Urusi imekuwa ikiitumia Iran kwa masilahi tu, na si kwamba kuna ‘urafiki wa kweli’.

“‘… wanasiasa wa Urusi hawaipendi Iran, bali wanaiona kama fursa tu,” anasema Smagin.

Wakati huo huo, mchambuzi kutoka Taasisi ya Chatam House ya London, Gregoire Roos, anasema Urusi inaitumia Iran kujifunza baadhi ya mambo.

Roos anasema Urusi inakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kutoka kwa mataifa ya Magharibi, hivyo inaitumia Iran kujifunza namna ya kuishi navyo.

“Iran ina uzoefu wa miaka mingi wa kukabiliana na vikwazo vya kimataifa, hivyo imekuwa ikiisaidia Urusi njia za kukabiliana navyo,” anasema Roos.

Katika hatua nyingine, wachambuzi wanakubaliana kuwa ni ngumu kwa Urusi kuingilia vita ya sasa kwa kuwa haikuingia makubaliano ya ushirikiano wa masuala ya ulinzi na Iran.

Aidha, baadhi ya wachambuzi wanaamini kitendo cha Urusi kutoingia vitani kuisaidia Iran kinaweza kuathiri, kama si kuisambaratisha kabisa, uhusiano uliopo kati ya mataifa hayo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img