23.5 C
New York

Zuhura ahimiza wafanyakazi kushiriki michezo ili kujenga afya

Published:

Mwandishi Wetu, Gazetini-Singida

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunus, amewahimiza wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini kujenga utamaduni wa kushiriki michezo na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya zao na kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, ambayo amesema yamekuwa changamoto kubwa kwa watu duniani kote.

Zuhura ametoa wito huo jana wakati wa hafla ya kufunga Bonanza la Michezo la OSHA lililoandaliwa na kuratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, yaliyofanyika katika viwanja vya Mandewa, mkoani Singida.

Akizungumza katika hafla hiyo, Zuhura amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikihamasisha wananchi kuzingatia umuhimu wa michezo na mazoezi katika kujenga afya bora na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa asilimia 75 ya vifo vinavyotokea kila mwaka duniani husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza. Hapa nchini, Wizara ya Afya inakadiria kuwa kati ya vifo 100 vinavyotokea kila mwaka, vifo 33 vinasababishwa na magonjwa hayo. Hivyo, nawasihi wafanyakazi wote kuepuka mtindo wa maisha usiofaa na kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara,” alieleza Zuhura.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akisisitiza umuhimu wa wafanyakazi kushiriki michezo wakati akizungumza na washiriki wa Bonanza la OSHA lililofanyika Mkoani Singida.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema lengo kuu la bonanza hilo ni kuhamasisha wafanyakazi kushiriki katika michezo kwa ajili ya kujenga afya bora na kuimarisha mshikamano baina yao. Aidha, alieleza kuwa OSHA itaendelea kulinda nguvu kazi ya taifa kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali, zikiwemo kaguzi za usalama na afya mahali pa kazi, ili kuhakikisha wafanyakazi wanatekeleza majukumu yao wakiwa salama na wenye afya njema.

Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mbio za magunia, riadha, mbio za vijiti, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, na mchezo wa kukimbia na ndimu. Katika mashindano hayo, OSHA ilitwaa ubingwa katika mchezo wa mpira wa pete na riadha kwa wanaume na wanawake, huku timu ya OSHA Sports Club ikifikia hatua ya nusu fainali katika mchezo wa mpira wa miguu.

Timu za wafanyakazi kutoka maeneo mbalimbali ya kazi nchini zikishiriki katika michezo tofauti tofauti katika Bonanza la OSHA lililofanyika katika Viwanja vya VETA Mkoani Singida.

Timu zilizoshiriki katika bonanza hilo ni pamoja na timu kutoka: OSHA, Wizara ya Ujenzi, Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM), Wizara ya Uchukuzi, Mahakama, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Bohari ya Dawa (MSD), TANROADS, Shanta Gold Mine, Wizara ya Afya, Benki ya NMB, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img