RIO, Brazil
HIVI karibuni, lejendari wa soka la Uholanzi aliyewahi kuwika na AC Milan, Clarence Seedorf, alitua Ligi Kuu ya Brazil, ambako amekabidhiwa mikoba ya kuinoa Corinthians.
Hivyo, Seedorf anakuwa kocha wa staa wa zamani wa Manchester United, Jesse Lingard, ambaye anaitumikia klabu hiyo kongwe katika soka la Brazil.
Hata hivyo, Lingard si mchezaji pekee mkubwa anayecheza Brazil baada ya kuwika barani Ulaya.
Saul Niguez
Wakati fulani, Niguez alikuwa mchezaji muhimu wa Atletico Madrid, kiasi cha klabu hiyo kumpa mkataba mrefu wa miaka tisa. Ni timu aliyoanza nayo tangu akiwa kinda.
Baadaye, alizitumikia Chelsea na Sevilla kwa mkopo, kabla ya Atletico kuamua kuachana naye moja kwa moja. Niguez alitua Flamengo ya Brazil mwaka 2025 na ametwaa mataji makubwa mawili [Copa Libertadores na Serie A].
Hulk
Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 40, Hulk bado anakipiga. Straika huyo wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya Brazil aliwahi kupita Japan, Ureno, Urusi na China.
Kwa sasa, anaitumikia Fluminense ya Brazil aliyojiunga nayo Mei, 2026, na mkataba wake utafikia ukomo mwaka 2027. Alisajiliwa na Fluminense baada ya miaka mitano ya kuitumikia klabu nyingine kubwa ya Brazil, Atletico Mineiro.
Martin Braithwaite
Ni mchezaji wa zamani wa Middlesbrough na Barcelona, pia akiwahi kupita katika klabu mbalimbali za Denmark na Ufaransa. Braithwaite [35], anakipiga Gremio aliyojiunga nayo mwaka 2024 baada ya kuondoka Espanyol.
Braithwaite alisajiliwa kuziba pengo la Luis Suarez aliyehamia Marekani. Ameshafunga mabao 27 tangu aliposajiliwa na klabu hiyo.
Fred
Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil aliwahi kucheza Ligi Kuu ya England [EPL] akiwa na Manchester United. Alipoondoka Old Trafford, aliitumikia Fenerbahce kwa miaka mitatu.
Kwa sasa, Fred anakipiga Atletico Mineiro. Ni klabu ambayo aliitumikia kwa miaka sita mwanzoni mwa maisha yake ya soka. Kabla ya kwenda Ulaya na kuwa staa.
Hakim Ziyech
Akiwa katika ubora wake, kiungo wa pembeni huyo raia wa Morocco aliwahi kukipiga Ajax ya Uholanzi na baadaye Chelsea ya Ligi Kuu nchini England.
Alipita kwa nyakati tofauti Galatasaray ya Uturuki, Al-Duhail ya Qatar na Wydad ya Morocco. Kwa sasa, ana miaka 33 na anakipiga Botafogo aliyojiunga nayo Septemba, 2026.
Alex Telles
Ndiye nahodha wa Botafogo anayoitumikia Ziyech. Telles aliyetua Brazil akitokea Ligi Kuu ya Saudi Arabia, aliwahi kucheza Ulaya akiwa na Porto na Manchester United.
Beki wa kushoto huyo alisajiliwa na Botafogo mwaka 2024 na miezi michache baadaye alifunga bao wakati timu hiyo ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Kusini mwa Amerika [Copa Libertadores].
Lucas Moura
Winga wa zamani wa Tottenham. Alirejea nyumbani [Brazil] mwaka 2023 na kujiunga na klabu ya Sao Paulo. Alisajiliwa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Tottenham.
Mkataba wake wa sasa utakwisha mwishoni mwa mwaka huu, 2026, na tayari ameshaifungia mabao 25 katika mechi 109 alizocheza kwenye michuano mbalimbali.
Cedric Soares
Alicheza Ligi Kuu ya England kwa takribani miaka 10 akiwa na Southampton, Arsenal na Fulham. Arsenal waliachana naye mwaka 2024 na Sao Paulo walimsajili mwaka uliofuata.
Tangu aliposajiliwa, amekuwa akipata nafasi kubwa ya kucheza, tofauti na alivyokuwa akisota benchi pale Emirates.
Alex Sandro
Akiwa kwenye ubora wake, alikuwa miongoni mwa mabeki wa kushoto bora kuwahi kutokea Ligi Kuu ya Italia [Serie A], wakati huo akikipiga Juventus.
Sandro alicheza Ulaya kwa miaka 13, akianza na Porto, kabla ya kujiunga na Juventus mwaka 2015. Alipoondoka Juventus, alitua Flamengo na mkataba wake ni wa miezi 18 tu.
Memphis Depay
Ukiacha Lingard, Depay ni mchezaji mwingine wa zamani wa Man United anayecheza Corinthians ya kocha mpya, Seedorf. Depay alitua klabuni hapo mwaka 2024 baada ya kuondoka Atletico Madrid.
Hata hivyo, Mholanzi huyo amekuwa kwenye uhusiano usio na afya na mabosi wake. Wakati fulani, aliwajia juu akisema wameshindwa kuheshimu makubaliano ya kumpa mkataba mpya.


