24.6 C
New York

Ndejembi: Ushikiano wa Tanesco na CRDB utaongeza kasi ya uunganishaji umeme

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amesema Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Benki ya CRDB, unalenga kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kupata huduma ya umeme kwa urahisi na kwa wakati, ili kuongeza fursa za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza leo, Oktoba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya utiaji saini na uzinduzi wa mpango huo, Makamu wa Rais amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kutekeleza Mpango wa Misheni 300, unaolenga kuhakikisha hadi mwaka 2030 wananchi milioni 300 barani Afrika wanafikiwa na nishati ya umeme.

Amesema kupitia ushirikiano huo, wananchi wanaostahili watanufaika na utaratibu wa kugharamiwa gharama za uunganishaji wa umeme, hatua ambayo inalenga kuongeza kasi ya kuzifikia kaya takribani milioni 1.7 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact).

“Ninaipongeza Tanesco na Benki ya CRDB kwa hatua hii muhimu ya kuanzisha ushirikiano unaolenga kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya umeme. Ushirikiano huu ni mfano bora wa namna taasisi za umma na sekta binafsi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali ili kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja,” amesema Ndejembi.

Serikali yapongeza ushirikiano

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dk. Juma Homera, amepongeza hatua hiyo, akisema kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, wananchi wataendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuwafikishia huduma muhimu ya umeme.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Balozi Zuhura Bundala, amesema utekelezaji wa ushirikiano huo ni matokeo ya Serikali, chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuweka mazingira wezeshi ya kukuza fursa za kiuchumi na kijamii kupitia nishati ya umeme.

“Tunatarajia mpango huu uweze kuwafikia wananchi wengi, ambao tunaamini watanufaika na fursa mbalimbali ikiwemo ajira, uzalishaji, biashara na kuwezesha mazingira bora katika sekta ya elimu,” amefafanua Balozi Bundala.

Vijijini kupata Ufadhili wa Shilingi 27,000

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema kupitia makubaliano hayo, awamu ya kwanza inalenga maeneo ya vijijini, ambapo Benki ya CRDB itawezesha kiasi cha shilingi 27,000 kwa kila kaya inayostahili.

Amesema fedha hizo zitalipwa moja kwa moja kwa Tanesco kama gharama za uunganishaji wa umeme, bila mwananchi kuwa na wajibu wa kuzirejesha.

Kwa wananchi wa mijini na pembezoni mwa miji, Twange amesema CRDB itawezesha upatikanaji wa fedha kupitia mikopo nafuu, ambayo italipwa kwa utaratibu utakaowekwa na benki hiyo.

“Mpaka sasa Tanesco ina takribani wateja milioni 6.4, lakini kupitia mpango huu wa ushirikiano tunatarajia idadi ya wateja itaongezeka na kufikia lengo la kuunganisha kaya milioni 1.7 kwa mwaka,” amesema Bw. Twange.

CRDB yatenga bilioni moja kwa mwaka

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imetenga shilingi bilioni moja kila mwaka kwa ajili ya mpango huo.

Amesema CRDB, kwa kushirikiana na Tanesco, itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia fursa hiyo muhimu katika kusukuma mbele maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Kupitia Mpango wa Kitaifa wa Nishati (National Energy Compact), Tanzania imelenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme kutoka asilimia 78.4 hadi asilimia 100, pamoja na kuongeza kiwango cha wananchi waliounganishwa na umeme kutoka asilimia 46 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030.

Related articles

Recent articles