MANCHESTER, Uingereza
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester City, Sergio Aguero, amempa onyo kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, akimtaka kuwa makini na mtindo wake wa kubadili kikosi mara kwa mara.
Kama alivyokuwa akifanya Pep Guardiola, Arteta amekuwa akigawa wachezaji, ambapo baadhi hucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na wengine huwatumia kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Aguero, mtindo huo huweza kuathiri saikolojia ya wachezaji wanaofanya vizuri.
“Tatizo ni kwamba wakati mwingine wachezaji walio kwenye kiwango kizuri hujisikia vibaya wanapoona wanawekwa benchi kwa ajili tu ya kupisha wengine wacheze,” amesema.
Baada ya kasi nzuri tangu kuanza kwa msimu huu, Arsenal walionja joto ya jiwe wikiendi hii baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Brighton.


