MIAMI, Marekani
LICHA ya kukosa ubingwa wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu (2026) baada ya kufungwa bao 1-0 na Hispania, nahodha wa timu ya soka ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, ameweka rekodi yake.
Ndoto ya Argentina kutetea taji walilobeba mwaka 2022 ziliota mbawa usiku wa jana Julai 19, 2026, baada ya Ferran Torres kuifunga Hispania bao la dakika ya 106.
Kwa mujibu wa mtandao wa takwimu wa OptaJoe, Messi anakuwa mchezaji wa kwanza kufika fainali ya Kombe la Dunia mara tatu mfululizo tangu Cafu wa Brazil alipofanya hivyo.
Pia, Messi (39), anakuwa mchezaji wa ndani mwenye umri mkubwa zaidi kucheza fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Mshindi huyo wa tuzo nane za Ballon d’Or, amemaliza msimu huu wa Kombe la Dunia akiwa amefunga mabao nane na kutoa ‘asisti’ nne.


