ADIS ABABA, Ethiopia
RAIA wa Ethiopia wameingia kwenye Uchaguzi Mkuu Juni Mosi, 2026, huku mambo matatu yakiteka mijadala mingi katika siasa za nchi hiyo.
Ifahamike kuwa huu unakuwa Uchaguzi wa saba nchini humo tangu kuanguka kwa utawala wa kijeshi mwaka 1991.
Wapiga kura watachagua wabunge 547 na Chama kitakachopata walau kura 274 ndicho kitakachounda Serikali na kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Mosi, Ethiopia imeingia kwenye Uchaguzi wakati huu hali ya usalama ikiwa mbaya katika maeneo mengi, ukiwamo Mkoa wa Kaskazini wa Tigray, ulioondoshwa katika Uchaguzi.
Itakumbukwa kuwa viongozi wa Tigray waliingia kwenye vita na Serikali mwaka 2020 na kusababisha vifo vya watu 600,000.
Ukiacha kinachoendelea Tigray, mikoa miwili yenye watu wengi zaidi, Amhara na Oromia, nayo inakabiliwa na machafuko yasiyokoma.
Wapiganaji wa Fano mkoani Amhara na Oromo Liberation Army (OLA) wa Oromia wameendelea kuvipa wakati mgumu vyombo vya dola.
Pili, hali ya uhuru wa vyombo vya habari inatiliwa shaka, ambapo hata Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limenyimwa kibali cha kuripoti Uchaguzi Mkuu huo.
Katika ripoti ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka, Ethiopia iko hoi kwa uhuru wa vyombo vya habari, ikishika nafasi ya 148 katika nchi 180.
Mwaka 2025, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch lililaani matukio ya waandishi kukamatwa na kunyanyaswa nchini Ethiopia.
Tatu, Chama cha Prosperity Party ndicho kinachopewa nafasi kubwa ya kushinda. Ni Chama cha Waziri Mkuu wa sasa, Abiy Ahmed.
Abiy (49), aliingia madarakani mwaka 2018 kupitia Chama cha Ethiopian People’s Revolutionary Democratic Front (EPRDF) kilichokuwa kikiundwa na wanasaisa wengi kutoka Tigray.
Alipoingia madarakani, aliivunja EPRDF na kuanzisha Chama chake, Prosperity Party, ambacho ndicho kilichoongoza nchi kwa sasa.
Hata hivyo, kwa wakosoaji, Uchaguzi wa Mwaka huu ni kiini-macho tu kwani tayari Chama cha Prosperity kimeendaaliwa mazingira ya kushinda.
Mwanasiasa mkongwe wa upinzani, Prof. Merera Gurdina, anasema: “Tunashiriki tu kwa sababu sheria zinakataza kugomea Uchaguzi. Tunashiriki ili kuepuka kufutiwa usajili.”
Wakosoaji wengi, akiwamo Prof. Gurdina, wanamuona Waziri Mkuu Abey ni mtu tofauti na alivyoingia madarakani miaka nane iliyopita na kushinda tuzo ya Amani ya Nobel (2019).
Mwisho, licha ya hali tete ya usalama katika baadhi ya maeneo, Ethiopia, Taifa la pili barani Afrika kwa idadi ya watu (milioni 135.9) baada ya Nigeria, inafanya vizuri kiuchumi, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.
Mathalan, Pato la Taifa (GDP), ambalo hupimwa kwa wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja, linatarajiwa kufikia Dola 1.133 mwaka 2016, ikilinganishwa na Dola 641 mwaka 2016.


