Na mwandishi wetu, Gazetini
KIUNGO wa Vipers SC ya Uganda, Abdu Karim Watambala, ameingia kwenye rada za klabu ya Simba, inayompigia hesabu za kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine.
Watambala ametoka kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka msimu wa 2025-26 wa Ligi Kuu ya Uganda uliomalizika hivi karibuni kwa klabu yake kutwaa ubingwa.
Nyota huyo alitwaa tuzo hiyo akiwapiku Frank Ssebufu na Raymond Barasa Mangoli (SC Villa), Ivan Ahimbisibwe (KCCA FC) na Ambrose Kigozi (Entebbe UPPC).
Tuzo hiyo imetokana na kiwango chake bora msimu huo, ambao aliumaliza akiwa amezifumania nyavu mara 12 na kutoa pasi zilizozaa mabao manne.
Nyota huyo anafahamiana vizuri na nyota wa Yanga, Allan Okello, ambaye si tu ni Mganda mwenzake, bali pia walikuwa wakicheza pamoja katika kikosi cha Vipers.
Baada ya Yanga kumchukua Okello, ndipo benchi la ufundi la Vipers lilipompa Watambala majukumu ya kucheza eneo lake la kiungo mshambuliaji (namba 10).
Ikumbukwe, wakati Okello akicheza nafasi hiyo, Watambala alikuwa akitumika kama kiungo wa kati (namba 8) katika kikosi hicho.
Tangu ahamie namba 10, Watambala amekuwa kwenye kiwango bora, ikichagiwa na uwezo wake wa kufunga, kutengeneza nafasi na kutoa ‘asisti’.
Vipers ilimsajili msimu wa 2019-20 baada ya kumaliza elimu ya sekondari. Katika msimu wake huo wa kwanza, akawa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uganda.
Pia, Watambala anayetumia zaidi mguu wa kushoto, alionesha kiwango bora wakati wa michuano ya CHAN ya mwaka 2019, hivyo kuitwa timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’.
Alicheza kwa mara ya kwanza akiwa na Cranes mwaka 2020, akitokea benchi katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sudan Kusini, mchezo wa kuwania tiketi ya fainali za AFCON 2021.
Msimu wa 2023-24, Watambala alikuwa na kiwango bora lakini kumbukumbu kwa mashabiki wa Vipers ni bao aliloifunga BUL FC na kuiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Je, Wekundu wa Msimbazi watafanikisha usajili wake? Na je, ikiwa atatua, atawika Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa Okello na Khalid Aucho?


