DAKAR, Senegal
IJUMAA ya wiki hii, Mei 22, 2026, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, alimfuta kazi Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko, hatua iliyoambatana na kulivunja Baraza la Maawziri.
Taarifa ya Sonko ‘kutumbuliwa’ haikuwashitua wengi, pia ikipokelewa kwa furaha na Waziri Mkuu huyo akisema walau sasa atapata usingizi.
“Alhamdulillah (Asante Mungu). Usiku wa leo nitalala vizuri nikiwa kwangu Keur Gorgui,” aliandika Sonko kupitia ukurasa wa Facebook, muda mfupi tu baada ya kupoteza kibarua
Wakiwa marafiki wakubwa, wanasiasa hao (Rais Faye na Waziri Sonko) waliingia madarakani mwaka 2024, wakiahidi mapinduzi makubwa katika nyanja za siasa na uchumi nchini Senegal.
Wakati huo wakiungwa mkono na wananchi wengi, Faye na Sonko walikosoa uongozi uliopita wakitaja vitendo vya rushwa kusababisha Taifa hilo la Afrika Magharibi kuelemewa na mzigo wa madeni ya nje.
Hata hivyo, kwa miezi ya hivi karibuni, uhusiano kati yao umekuwa mbaya na wa kutiliwa shaka. Wiki chache zilizopita, Sonko alimshutumu Rais Faye kwa madai kuwa amekuwa ‘dikteta’ ndani ya Chama tawala, Pastef.
Kwa upande mwingine, Sonko alienda mbali zaidi na kumtaja Rais Faye kuwa ni kiongozi aliyefeli kumlinda dhidi ya wakosoaji wake.
Rais Faye alijibu madai hayo kupitia mahojiano yake na kituo cha televisheni, akisema: “Yeye ni Waziri Mkuu kwa sababu mimi ndiye niliyetaka. Kama nitaamua, atapatikana Waziri Mkuu mpya.”
Rais Faye na Soko walipoingia madarakani mwaka 2024, waliikuta Senegal ikiwa na uchumi uliomezwa na madeni ya nje.
Kwa miaka miwili ya kuongoza, bado nchi hiyo inashika nafasi ya pili kwa madeni, kwa mujibu wa takwimu za Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mwaka 2025, Sonko alidai kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) lilitaka kukaa mezani na Senegal kuangalia namna ya kupunguza deni, hatua ambayo alisema Rais Faye aliikataa.
Hata hivyo, Aprili, 2026, Rais Faye alitangaza kuwa atashughulikia mwenyewe mazungumzo na IMF ili kujadili suala la deni hilo.
Aprili, 2026, Bunge la Senegal lilipitisha muswada unaomruhusu Sonko kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2029. Ni Uchaguzi ambao Rais Faye atakuwa akiwania muhula wake wa pili.


