13.5 C
New York

Sajili hizi zimelipa, zimerudisha chenji EPL 2025-26

Published:

LONDON, Uingereza

UKIWEKA kando Arsenal kutwaa ubingwa, msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeshuhudia viwango bora vya wachezaji waliosajiliwa na klabu mbalimbali.

Nyota hao ni wale waliosajiliwa kwa ajili ya msimu huu, yaani wale wa kiangazi, 2025, hadi Januari, 2026. Makala haya yanachambua.

RAYAN CHERKI (MAN CITY)

Amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Man City tangu aliposajiliwa kwa Pauni milioni 30.5 akitokea AC Milan ya Italia.

Akiwa na asisti 12, Cherki amezidiwa na Bruno Fernandes pekee msimu huu. Mbali ya asisti, pia nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 amefunga mabao manne.

GRANIT XHAKA (SUNDERLAND)

Ilishangaza wengi kuona kiungo huyo wa zamani wa Arsenal akiondoka Bayer Leverkusen na kutua Sunderland. Diki hilo liligharimu Pauni milioni 17.

Kwa ubora wa pasi, sambamba na asisti zake sita, ni wazi Sunderland walikuwa sahihi kumsajili na kumpa kitambaa cha unahodha.

SENNE LAMMENS (MAN UNITED)

Baada ya kumkosa Emiliano Martinez wa Aston Villa, Manchester United waliamua kumsajili Lammens kwa ada ya Pauni milioni 18 akitokea Royal Antwerp.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 23, ameonesha uwezo mkubwa na ubora wake langoni umechangia Man United kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao (2026-27).

DOMINIC CALVERT-LEWIN (LEEDS UNITED)

Alifunga mabao 17 tu katika misimu minne aliyocheza Everton, hiyo ikitokana na wimbi la majeraha kwa Muingereza huyo.

Hata hivyo, Calvert-Lewin ni kama ‘amezaliwa upya’ akiwa Leeds aliyojiunga nayo akiwa mchezaji huru. Amefunga mabao 14 akibakiza mchezo mmoja kumaliza msimu huu.

JOAO PEDRO (CHELSEA)

Usajili uliogharimu Pauni milioni 60 akitokea Brighton. Msimu wake wa kwanza Stamford Bridge umekuwa na mafanikio makubwa.

Mbrazil huyo amehusika katika mabao 20 ya Chelsea na haikushangaza alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka klabuni hapo.

ANTOINE SEMENYO (MAN CITY)

Man City walitumia Pauni milioni 62.5 kumng’oa Bournemouth. Alifunga mabao matano katika mechi zake saba za mwanzo akiwa na matajiri wa Etihad.

Licha ya kwamba upepo wa kufunga umepotea kwa kiasi fulani, bado Semenyo ni mchezaji wa kikosi cha kwanza chini ya kocha Pep Guardiola.

GIANLUIGI DONNARUMMA (MAN CITY)

Kipa huyo raia wa Italia alitua Etihad baada ya mabosi wa klabu ya Man City kuipa PSG kitita cha Pauni milioni 26.

Kwa sasa, ndiye kinara wa kuokoa mabao (72.9%) kwenye Ligi, pia amecheza mechi 15 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

VICTOR GYOKERES (ARSENAL)

Usajili ulioigharimu Arsenal kitita cha Pauni milioni 55 akitokea Sporting Lisbon ya Ureno.

Kuelekea mechi ya mwisho wikiendi hii, ameshafunga mabao 14 ya kwenye Ligi Kuu, akiwa amezidiwa na wachezaji wanne tu.

MARTIN ZUBIMENDI (ARSENAL)

Pauni milioni 56 ziliitoka Arsenal kumng’oa kiungo huyo katika kikosi cha Real Sociedad ya Liga. Usajili huo umelipa.

Zubimendi ametengeneza ‘pacha’ nzuri ya safu ya kiungo ya Arsenal akiwa na Declan Rice, pia amefunga mabao matano msimu huu wa Ligi.

HUGO EKITIKE (LIVERPOOL)

Liverpool walialazimika kutumia Pauni milioni 69 kumng’oa mshambuliaji huyo katika kikosi cha Eintracht Frankfurt ya Bundesliga.

Kabla ya kupata majeraha yatakayomrejesha msimu ujao, Mfaransa huyo alishafunga mabao 11 n kutoa asisti nne kwenye Ligi.

Related articles

Recent articles