MANCHESTER, Uingereza
PEP Guardiola anaondoka Manchester City, klabu aliyoinoa kwa mafanikio makubwa tangu ilipomuajiri mwaka 2016 akitokea Bayern Munich ya Bundesliga.
Kwa upande mwingine, miaka yake 10 imemfanya Guardiola kuwa kinara wa matumizi ya fedha katika soko la usajili, akitumwaga Pauni bilioni 1.7 kunasa wachezaji 37.
Hata hivyo, Mhispania huyo anaondoka Etihad akiwa na kumbukumbu ya kuumiza ya kuwakosa wachezaji wakubwa watano aliowahi kutaka wasajiliwe.
LUCAS PAQUETA
Kiungo huyo wa kimataifa wa Brazil ni kipenzi cha Guardiola na alikaribia kutua Man City mwaka 2023 akitokea West Ham United ya Magharibi mwa Jiji la London.
Guardiola aliamini Paqueta alikuwa mchezaji sahihi wa kuziba pengo la Kevin De Bruyne aliyekuwa amejiunga na Napoli ya Serie A.
Hata hivyo, licha ya Man City kukubali kuweka mezani Pauni milioni 68, dili hilo liliota mbwa dakika za mwisho baada ya Paqueta kufunguliwa mashitaka ya kubeti.
BRUNO GUIMARAES
Baada ya Rodri kupata majeraha ya goti, Guardiola aliamini Bruno Guimaraes anapaswa kusajiliwa ili kuziba pengo la Mhispania huyo.
“Nimekuwa shabiki mkubwa wa Bruno. Tangu akiwa Lyon, alionekana ni mchezaji tofauti. Newcastle walifanya usajili wa maana,” alisema Guardiola mwaka 2025.
Licha ya sifa hizo, kocha huyo hakufanikiwa kumsajili Guimaraes na sasa anaondoka akiwa hajatimiza ndoto ya kufanya kazi na mchezaji anayemkubali.
JORGINHO
Mwaka 2018, Guardiola alimtaka kiungo huyo wa kimataifa wa Italia. Man City walipeleka ofa yao kwa Napoli, ikitajwa kuwa ni Pauni milioni 43.
Hata hivyo, klabu hiyo ya Italia iligoma na Chelsea ikafanikiwa kumsajili.
Taarifa zinaeleza kuwa kocha wa Blues wakati huo, Maurizio Sari, ambaye naye alitokea Napoli, ndiye aliyemshawishi kuikataa Man City ha kutua Stamford Bridge.
Guardiola alisema: “Kwa Jorginho, lingekuwa kosa kubwa kwake na kwetu pia kuja hapa Etihad wakati alitaka kumfuata Maurizio.”
FRED
Baada ya Fred kuonesha kiwango kizuri katika mchezo ambao Man City ilisinda mabao 4-1, Guardiola alivutiwa na kiungo huyo aliyekuwa na kikosi cha Shakhtar Donetsk.
Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya Man City na Shakhtar yalifanyika na kukubaliana juu ya usajili wa Pauni milioni 34.
Lakini, mambo yalibadilika ghafla baada ya Manchester United kufika mezani na ofa nono zaidi ya Pauni milioni 50. Fred akatua Old Trafford.
HARRY KANE
Mwaka 2021, Guardiola alipanga kuiongezea makali safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili Kane. Man City ilifika na ofa nzuri ya kitita cha Pauni milioni 100.
Lakini, Tottenham iligoma kumwachia straika huyo na hatimaye alitimkia Bayern Munich. “Tulijaribu kumsajili Kane lakini Tottenham iliweka wazi kuwa hauzwi.
Mwishowe, Kane alitimkia Bayern Munich na sasa ni kinara wa mabao Bundesliga na ni miongoni mwa washambuliaji wa kiwango cha juu katika soka la Ulaya.


