CAIRO, Misri
MAMELODI Sundowns ya Afrika Kusini dhidi ya vigogo wa soka la Morocco, FA Rabat, katika mtanange wa kukata na shoka wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Mei 15, 2026.
Kama ilivyo kawaida, zitachezwa fainali mbili (nyumbani na ugenini), ambapo mechi ya marudiano itakuwa wiki moja baada ya hiyo ya kwanza.
HAWA HAPA FAR RABAT
FAR Rabat wanasaka taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa tangu walipolinyakua mwaka 1985 kwa kuifunga AS Bilima ya DRC. Hii ni fainali yao ya kwanza tangu wakati huo.
Katika raundi ya kwanza na ya pili msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, walizitoa Real de Banjul ya Gambia (4-1) na Horoya ya Guinea (4-0).

Walipoingia makundi, walianza vibaya kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga, kabla ya kushinda mechi mbili na kutoa sare tatu, wakishika nafasi ya pili kwenye Kundi B, nyuma ya Al Ahly.
Robo fainali walikutana na mabingwa watetezi, Pyramids, ambapo waliwatoa kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2.
Hatua ya nusu fainali iliwakutanisha na vigogo wenzao wa soka la Morocco, RS Berkane, na kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-1.
Uwanja wa nyumbani ndiyo silaha kubwa ya FA Rabat. Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa, wamepoteza mechi moja pekee tangu mwaka 2023. Wameshinda 13 na kutoa sare tatu.
MAMELODI NAO VIPI?
Hii ni nafasi nyingine kwa Mamelodi baada ya kupoteza fainali ya msimu uliopita walipofungwa na Pyramids ya Ligi Kuu nchini Misri.
Safari hii, ‘Masandawana’ walifika fainali kwa kuing’oa Esperance de Tunis. Mechi ya kwanza ilichezwa Tunisia na Memelodi kushinda bao 1-0, matokeo waliyoyapata pia katika mchezo wa marudiano mjini Pretoria, Afrika ya Kusini.
Vigogo hao wa Ligi Kuu ya ‘Sauzi’ wamekuwa kwenye mawindo ya taji la Ligi ya Mabingwa kwa miaka 10 na kwa sasa kocha wao ni raia wa Ureno, Miguel Cardoso.
Cardoso ambaye hajawahi kutwaa taji hilo, licha ya kwamba ameshawahi kufika fainali mara mbili akiwa na timu mbili tofauti; Esperance na Mamelodi.


