9.5 C
New York

Mhasibu afikishwa Kisutu kwa mashtaka 43 ya uhujumu uchumi

Published:

Na Imani Nathaniel, Dar es Salaam

Mhasibu Hamid Ahmed Hussein, mkazi wa Ocean Road jijini Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na jumla ya mashtaka 43 yakiwemo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Franco Kiswaga, Wakili wa Serikali Cathbet Bilinyi alidai kuwa mtuhumiwa alitenda makosa mbalimbali ya kughushi nyaraka, kutumia nyaraka za uongo na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika maeneo ya Mikocheni, wilayani Kinondoni.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa katika nyakati tofauti kati ya Januari 2020 na Februari 2026 , mtuhumiwa alighushi nyaraka mbalimbali zikiwemo stakabadhi na hati za malipo (levy), akizionyesha kuwa zimetolewa na Manispaa ya Temeke ilhali si za kweli.

Aidha, ilidaiwa kuwa kupitia nyaraka hizo za kughushi, mtuhumiwa alifanikiwa kujipatia fedha kutoka kampuni ya Kutoka Kampuni binfsi ambapo kiasi kinachotajwa katika mashtaka mbalimbali kinafikia mamilioni ya shilingi, huku jumla ya fedha zinazodaiwa kuhusika zikitajwa kufikia hadi shilingi bilioni tano.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa mtuhumiwa alijihusisha na miamala ya kifedha yenye lengo la kuficha asili ya fedha hizo zinazodaiwa kupatikana kwa njia haramu.

Hakimu Kiswaga amesema kuwa kosa la utakatishaji fedha halina dhamana na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo katika hatua ya sasa.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi Josephat Mabula alidai kuwa mteja wake amekaa mahabusu kwa siku 23 tangu akamatwe, akiiomba mahakama kuzingatia haki ya msingi ya mtuhumiwa na kutoruhusu ucheleweshaji wa kesi kutokana na sababu za upelelezi.

Hata hivyo, mahakama ilielekeza upande wa upelelezi kukamilisha uchunguzi wake kwa haraka ili mtuhumiwa aweze kufahamu hatma ya shauri lake.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 9 April mwaka huu huu kwa ajili ya kutajwa tena.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img