LONDON, Uingereza
KICHAPO cha mabao 3-0 kutoka kwa Everton kimeendeleza wimbi baya linaloiyumbisha Chelsea.
Kabla ya kupoteza mchezo huo wa Ligi Kuu, Blues iliondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kichapo cha jumla ya mabao 8-2 na PSG.
Kwa ufupi, sasa kocha Liam Rosenior amewashuhudia vijana wake wa Stamford Bridge wakikosa ushindi katika mechi nne mfululizo.
Huku msimu huu ukiwa imebakiza mechi saba pekee kwa kila timu, Chelsea iko nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi, hivyo kuna uwezekano wa kuikosa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Ukiweka kando kukosa matokeo mazuri, mashabiki wanaumizwa pia na ukame wa mabao, ambapo timu hiyo haijapasia nyavu katika mechi tatu mfululizo.
Aidha, mwenendo huo usioridhisha unatoa picha ya kile alichosema staa wa timu hiyo, Enzo Fernandes, kwamba Chelsea imepoteza uelekeo tangu ilipoachana na kocha Enzo Maresca.
Enzo raia wa Argentina, akaongeza kuwa hata wachezaji walishangaa kuona kocha huyo akifungashiwa virago Januari, 2026.
Hata hivyo, licha ya presha hiyo, Rosenior anasema: “Sijishughulishi na kelele hizo. Najua tulipo na tunachopaswa kufanya kama klabu.”


