27.7 C
New York

Usichokijua kuhusu saratani ya utumbo mpana

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SARATANI ya utumbo mpana inatajwa kuwa ndiyo aina ya saratani inayoongoza kwa idadi kubwa ya vifo kwa watu wenye umri chini ya miaka 50 nchini Marekani.

Mbaya zaidi, watatu kati ya wagonjwa wanne wa saratani ya utumbo mpana hubainika wakati tayari ugonjwa huo ukiwa imeshafikia hatua kubwa.

Mgonjwa anapogundulika wakati saratani ikiwa kwenye hatua kubwa, uwezekano wa kuishi miaka mitano umeshuka hadi asilimia 16, tofauti na asilimia 89 za awali.

Kwa mujibu wa utafiti wa Chama cha Ugonjwa wa Saratani cha Marekani (ACS), vifo vya vijana vitokanavyo na saratani zingine, ikiwamo saratani ya mapafu, vimepungua kwa asilimia 44.

Lakini, ndani ya miaka 30 ya hivi karibuni, saratani ya utumbo mpana imebaki kuwa tishio zaidi, ikiongoza kwa idadi kubwa ya vifo vya saratani zote.

Ripoti ya ACS inaonesha kuwa vifo vitokanavyo na saratani hiyo vimekuwa vikiongezeka kwa asilimia 1.1 kila mwaka tangu mwaka 2005.

Kwa kasi hiyo, saratani ya utumbo mpana inakuwa saratani inayoua zaidi, ikiipiku saratani ya mapafu iliyokuwa ikiongoza.

Kwanini vijana hatarini zaidi?

“Bado watafiti hawajafanikiwa kupata jibu, ingawa mifumo ya maisha ya vijana inaweza kutiliwa shaka,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa ACS, Arif Kamal.

Katika maelezo yake, Kamal anasema vijana, hasa wa Marekani, si watumiaji wa mboga za majani na matunda katika milo yao. “Pia, ni watumiaji wakubwa wa nyama nyekundu (ng’ombe, mbuzi, n.k),” anasema.

Kwa dalili hizi, wahi hospitali

Wataalamu, kupitia utafiti wa mwaka 2024, wanaeleza kuwa huchukua miezi minne hadi sita kwa dalili kujitokeza kwa mgonjwa.

Baadhi ya dalili za awali ni maumivu ya tumbo, kinyesi chenye damu, kuhairisha/kukosa choo, kupungua uzito na uchovu wa mara kwa mara.

Hata hivyo, mtaalamu wa afya, Lynn Durham, ambaye pia ni Rais wa Taasisi ya Saratani ya Georgia CORE, anasema shida kwa vijana ni pale wanapohisi aibu kuzungumzia masuala binafsi, hasa mabadiliko ya haja kubwa.

“Ukiwa na mtoto, ni rahisi kuzungumzia kinyesi chake wakati wote. Kuzungumzia ‘amepata choo’ mara ngapi, cha aina gani, ni kawaida.

“Suala hilo huenda na umri. Watu hawataki kuzungumzia hali ya haja kubwa. Wanapata mara ngapi, wanapata kinyesi kikiwa na sifa zipi,” anasema Durham.

“Ukiona kuna tofauti katika hali ya kinyesi chako, ni vizuri ukawahi haraka kwa daktari ili kuona ni nini kinaendelea. Unatakiwa umuone daktari haraka.”

Related articles

Recent articles