Na mwandishi wetu, Gazetini
HUENDA ukawa unachukulia poa, lakini tabia ya kufuatilia kila anachoweka mpenzi wako wa zamani (ex) huko mitandaoni kunaweza kukusababisha matatizo ya kiafya.
Kwa mujibu wa utafiti mpya, kitendo hicho kinaweza kuathiri saikolojia kwa kuwa kumfuatilia ‘ex’ hurudisha kumbukumhu zinazoweza kukuumiza.
Utafiti huo wa Chuo Kikuu cha Stony Brook cha Marekani unaeleza kuwa wengi hutaka kujua wenza wao wa zamani wanaendeleaje na wako na nani, jambo ambalo si zuri kwa afya zao.
Kwamba inaweza kuwaacha na msongo wa mawazo na huzuni, hasa wanapogundua kuwa ex wao wanaendelea vizuri, tofauti na walivyokuwa pamoja.
“Kufuatilia kila anachochapisha ex wako mitandaoni kunaufanya ubongo uendelee kuwa na kumbukumbu juu yake, badala ya kumsahau,” anasema Joanne Davila, ambaye ni mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Stony Brook.



