MOSCOW, Urusi
UINGEREZA na washirika wake imedai kuwa sumu itokanayo na chura ndiyo iliyotumika kumuua kiongozi wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny.
Navalny alipoteza maisha akiwa anashikiliwa na mamlaka miaka miwili iliyopita na tangu hapo umegubika utata mwingi juu ya chanzo cha kifo chake.
Kwa mujibu wa Uingereza, sumu iliyotumiwa na mamlaka za Urusi kumuua inafahamika kwa jina la Epibatidine na inatokana na chura wanaopatikana Kusini mwa Amerika.
Hata hivyo, Urusi imeendelea kuziita taarifa hizo ni kuwa kampeni chafu dhidi ya Serikali ya Rais wake, Vladmir Putin.
“Epibatidine ni sumu inayopatikana katika ngozi ya chura hao wa Amerika Kusini, kwa mujibu wa mtaalamu wa sumu, Jill Johnson.
“Ni hatari mara 200, ukilinganisha na sumu zingine. Epibatidine si tu inapatikana kwa chura hao wa porini, bali pia inaweza kutengenezwa maabara.”
Akieleza inavyofanya kazi, Johnson anasema sumu hiyo husababisha misuli kusinyaa, kupooza, kupunguza mapigo ya moyo, kushindwa kupumua na mwishowe kifo.
Baada ya Navalny kufariki, maabara za Ulaya ziliibuka na ripoti iliyodai kuwa mwanasiasa huyo alipewa sumu.
Mamlaka za Urusi zimekanusha zikidai kuwa alifariki kwa kuanguka akiwa kwenye matembezi, mke wake aitwaye Yulia Navalnaya anaamini mumewe alikatishiwa uhai.
Kabla ya kufariki, tayari Navalny alishakuwa gerezani kwa miaka mitatu akikabiliwa na mashitaka kadhaa, yakiwamo ya uhaini.


