RABAT, Morocco
SHIRIKISHO la Soka la Morocco (FRMF) limeweka wazi mpango wake wa kuiandikia barua ya malalamiko Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kupinga kile kilichotokea katika mchezo wa fainali ya AFCON 2025.
Mechi hiyo ya Januari 18, 2026 ilisimama kwa zaidi ya dakika 10 baada ya wachezaji wa Senegal kutoka nje ya uwanja wakigomea penalti waliyopewa Morocco katika dakika ya 89.
Kwa mujibu wa FRMF, kitendo hicho kiliharibu fainali hiyo na kuwavuruga wachezaji wake, hali iliyosababisha kufungwa bao 1-0 na kukosa ubingwa wa michuano hiyo wakiwa wenyeji.
Tukio la penalti lilitokea baada ya mwamuzi kupitia teknolojia ya VAR kujiridhisha kuwa Brahim Díaz wa Morocco aliangushwa ndani ya boksi na beki wa Senegal.
Kocha wa Senegal, Thiaw, aliwashinikiza wachezaji wake kutoka uwanjani ili kuzuia Díaz kupiga penalti, ambayo hata hivyo aliipiga na kukosa.
Nje ya uwanja, hali pia iliripotiwa kuwa mbaya, ambapo mashabiki wa Senegal walitibuana na polisi.
Katika taarifa yake, FRMF ilieleza: “Hili halikubaliki. Kuona wachezaji wakigomea mchezo na kushuhudia vurugu ni jambo lisilovumilika katika soka. Ni wazi haikuwa sawa.”
Kwa upande wake, kocha wa Morocco, Walid Regragui, amekiita kitendo kilichofanywa na Senegal kuwa ni aibu kubwa kwa soka la Afrika.


