11.2 C
New York

Sadio Mane anavyoibeba mabegani Senegal

Published:

DAKAR, Senegal

WAKATI timu ya taifa ya Senegal inatwaa ubingwa wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kuifunga Misri mwaka 2021, Sadio Mane ndiye aliyefunga penalti ya ushindi.

Safari hii, ameiongoza tena kubeba taji hilo nchini Morocco, akiwa ndiye Mchezaji Bora wa mashindano yaliyofikia ukomo jana Januari 18, 2025. Senegal waliifunga Morocco bao 1-0, mfungaji akiwa ni Pape Gueye.

Ikumbukwe, bao pekee alilofunga katika dakika ya 78 dhidi ya Misri ndilo lililoiwezesha Senegal kufika hatua hiyo ya fainali.

Azua gumzo fainali

Tukio lililozua gumzo katika fainali hiyo ni lile la mchezo kusimama kwa dakika zaidi ya 10 kutokana na mgomo wa wachezaji wa Senegal baada ya Morocco kupewa penalti.

Ilikuwa ni dakika ya 89, ambapo mwamuzi alitasfiri kuwa ni penalti kitendo cha beki wa Senegal, El Hadji Malick Diouf, kumwangusha kwenye boksi mshambuliaji wa Morocco, Brahim Diaz.

Kocha wa Senegal, Pape Thiaw, aliwahamasisha wachezaji wake kutoka uwanjani kugomea uamuzi huo, kabla ya Mane kufanya kitendo cha kishujaa kwa kuwaomba warudi uwanjani kuendelea na mchezo.

Dakika 16 baada ya mvutano, Diaz alipiga na kukosa penalti hiyo iliyookolewa na kipa wa Senegal aliyewahi kupita Chelsea, Edouard Mendy.

Kwa upande mwingine, kitendo cha Mane kufanikiwa kuwashawishi wenzake kurudi dimbani na kuendelea na mchezo kimetafsiriwa kuwa ni nidhamu kubwa aliyonayo mshambuliaji huyo.

Akihojiwa na BBC, mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi, amesema: “Mane alijiongeza na kuwaomba wenzake kurudi uwanjani. Alifanikiwa.”

Mchezaji wa zamani wa Morocco, Hassan Kachloul, naye amejitokeza kumpongeza Mane kwa kitendo hicho. “Kama si Mane, soka la Afrika lingeingia kwenye aibu,” amesema.

Shujaa kutoka kijijini

Akiwa katika Kijiji cha Bambali mwaka 2005, Mane alikuwa na umri wa miaka 13 tu wakati Liverpool ikitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuifunga AC Milan.

Ikiwa ni miaka 20 tu imepita, kwa sasa Mane ni nembo ya soka la Senegal na tayari upo uwanja wa soka uliopewa jina lake katika Mji wa Sedhiou ulioko umbali wa kilometa 20 kutoka kwao, Bambali.

Maisha ya kawaida tu

Licha ya mafanikio makubwa aliyonayo, ikiwamo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa akiwa na Liverpool aliyocheza mechi 300, Mane ameendelea kuishi maisha ya kawaida.

“Hata (Mane) anapokuja, bado amekuwa mpole na kuishi maisha ya kawaida kama watu wa hali ya chini hapa Bambali,” anasema kiongozi wa soka nchini Senegal, Fode Boucar Dahaba.

Tukio lake kubwa zaidi ni lile la kwenda kufanya usafi katika vyoo vya msikiti baada ya Liverpool kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa kwa kuifunga Liverpool mabao 3-1.

“Alitaka iwe siri, hakutaka iwe kwa ajili ya kujionesha kwa watu,” anasema Abu Usamah Al-Tahabi, ambaye ni kiongozi wa msikiti huo wa Al Rahma.

Kubadili uamuzi wa kustaafu?

Mane (33), ameshaweka wazi kuwa hizi zilikuwa ni fainali zake za mwisho kuitumikia timu ya taifa. Nyota huyo ameshaifungia Senegal mabao 53 katika mechi zaidi ya 120.

Wakati huo huo, staa huyo wa Al Nassr ya Saudi Arabia ndiye aliyekuwa na mabao mengi katika kikosi cha Senegal iliyokata tiketi ya kufuzu AFCON 2025.

Kwa upande mwingine, Gueye aliyefunga bao la ushindi jana hakubaliani na wazo la Mane kutaka kupumzika, na badala yake anataka kuona akibaki kikosini.

“Tutajaribu kumshawishi abaki walau kwa michuano mwingine ijayo kwa sababu bado ni mchezaji muhimu kwetu,” amesema Gueye anayekipiga Villarreal.

Mbali ya Gueye, kocha wake, Pape Thiaw, naye amesema hakubaliani na uamuzi wa Mane kustaafu. “Nafikiri alichukua uamuzi huo kutoka moyoni lakini Taifa halikubaliani nao. Na mimi kama kocha, sikubali,” amesema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img