MADRID, Hispania
MSHAMBUALIJI wa Real Madrid, Kylian Mbappe, anaamini si sahihi kusema Xabi Alonso alifeli katika kibarua chake cha kuinoa timu hiyo.
Alonso alifungashiwa virago hivi karibuni na kwa sasa Madrid inahusishwa na makocha kadhaa wa kupewa benchi la ufundi mwishoni mwa msimu huu.
Kwa upande wake, Mbappe amekanusha taarifa zinazodai kuwa Mhispania huyo ameponzwa na uhusiano wake mbaya na baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa klabuni hapo.
“Zinatoka wapi hizo taarifa za uhusiano mbaya kati ya wachezaji na kocha? Si kweli kwamba Alonso hakufanikiwa. Kwa upande wangu, naamini atakuwa kocha mkubwa,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mbappe alisisitiza kuwa alikuwa na uhusiano mzuri na Alonso. “Kilichotokea kimetokea. Ni uamuzi wa klabu,” amesisitiza.


