8.4 C
New York

Carrick mikononi mwa Guardiola, atatoboa?

Published:

MANCHESTER, Uingereza

NI wikiendi hii, Januari 17, 2026, ambapo Michael Carrick atapata mtihani wake wa kwanza mgumu atakapoiongoza Manchester United kuikabili Manchester City.

Timu hizo zitakwaana katika mchezo wa Ligi Kuu ya England utakaochezwa Old Trafford, ambapo historia inaitambua kuwa ni ‘derby’ ya 198.

Carrick amekabidhiwa kuinoa Man United hadi mwishoni mwa msimu huu, uamuzi huo ukichukuliwa wiki moja tu baada ya kocha Ruben Amorim kufungashiwa virago.

Man United wataingia kwenye mchezo huo wakiwa nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, wakiwa wana pengo la pointi tatu kuingia ‘Top Four’.

Hata hivyo, Man United imeshinda mechi moja pekee kati ya sita zilizopita. Carrick anaikuta ikiwa imeshinda mechi moja tu kati ya sita za hivi karibuni. Sare nne na kufungwa moja.

Man City, baada ya kuuanza mwaka 2026 kwa sare tatu mfululizo, ‘walifufuka’ na kuibuka na ushindi wa mabao 10-1 dhidi ya Exeter City.

Pep Guardiola wametoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle United katika mchezo wa michuano ya Kombe la Ligi (EFL Cup).

Man United na Man City zitavanaa zikiwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea Septemba, mwaka jana, ambapo Guardiola na vijana wake walishinda mabao 3-0 pale Etihad.

Kuelekea mchezo huo, Carrick atawakosa Noussair Mazraoui (AFCON) na Matthijs de Ligt (majeraha ya mgongo), wakati huo pia kinda Shea Lacey anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Habari njema kwake ni kurejea kwa washambuliaji wake, Bryan Mbeumo na Amad Diallo, baada ya timu zao za taifa kuondoshwa kwenye michuano ya AFCON. Mbeumo raia wa Cameroon ndiye mfungaji bora wa Man United msimu huu, akiwa ameingia kambani mara saba.

Kwa upande wa Man City, Guardiola anatarajiwa kuwakosa Josko Gvardiol, Mateo Kovacic, John Stones, Ruben Dias, Oscar Bobb na Savinho, ambao ni majeruhi, huku Omar Marmoush akiwa hajarejea kutoka AFCON.

Kiwango bora cha mshambuliaji mpya wa Man City, Semenyo, kinaweza kuwa habari mbaya kwa mabeki wa Man United. Ameshafunga mabao matatu katika mechi nne alizokutana na ‘Mashetani Wekundu’.

Aidha, Man City inafahamika kwa ubora wa mastaa wake wengine, wakiwamo Rayan Cherki, Phil Foden na Erling Haaland, ambaye ndiye mchezaji wa Man City aliyehusika katika mabao mengi (11) dhidi ya Man United.

Vikosi: Man United – Lammens, Dalot, Maguire, Martinez, Shaw, Casemiro, Mainoo, Mbeumo, Fernandes, Cunha na Sesko.

Man City – Donnarumma, Nunes, Khusanov, Alleyne, O’Reilly, Rodri, Bernardo, Cherki, Foden, Semenyo na Haaland.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img