8.4 C
New York

AFCON 2025 … Misri yang’oka ikiacha rekodi 5

Published:

RABAT, Morocco

LICHA ya kuondoshwa katika fainali za Mataifa ya Afrika zinazoendelea huko Morocco, timu ya taifa ya Misri ‘Mafarao’ imeacha historia ya aina yake.

Misri wameishia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa bao 1-0 na Senegal ‘Simba wa Teranga’, mfungaji akiwa ni Sadio Mane.

Je, ni rekodi zipi wanazotambia Misri baada ya safari yao ya kwenda fainali kukwamishwa na Senegal?
Mosi, mshambuliaji wake, Mohamed Salah, aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kuzifunga timu 11 tofauti kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Timu ambazo Salah amezifunga kwa nyakati tofauti ni Ghana, Burkina Faso, DR Congo, Uganda, Guinea-Bissau, Morocco, Mozambique, Zimbabwe, Afrika Kusini, Benin na Ivory Coast. Nyota huyo wa Liverpool aliweka rekodi hiyo alipofunga katika ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ivory Coast.

Pili, Salah alifikisha mabao 11 ya AFCON, akiifikia idadi aliyokuwa nayo Hossam Hassan, ambaye ndiye kocha wake kwa sasa. Salah akawa pia mchezaji wa kwanza wa Misri kufunga bao katika misimu mitano mfululizo ya mashindano hayo.

Tatu, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1970, Misri ilifunga bao la mapema zaidi katika michuano ya AFCON.
Staa wake anayekipiga Manchester City, Omar Marmoush, alifunga bao la dakika ya nne katika mchezo wao dhidi ya Ivory Coast.

Nne, Misri imetolewa ikiwa imeweka rekodi ya kufika mara 17 hatua ya nusu fainali ya AFCON. Ni kama ilivyo kwa Nigeria pia.

Tano, kabla ya kutolewa, Hossam Hassan alikuwa ndiye kocha wa kwanza baada ya miaka 106 kuiongoza Misri kucheza mechi 19 bila kufungwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img