KAMPALA, Uganda
KUELEKEA Januari 15, 2026, ambayo ndiyo siku ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda, Serikali nchini humo inayoongozwa na Rais Yoweri Museveni imeagiza kuzimwa kwa mitandao.
Agizo la kuzimwa kwa intaneti limezigusa kampuni za mitandao ya simu, pamoja na wenye leseni za utoaji wa huduma za mawasiliano katika Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Aidha, agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano nchini Uganda (UCC) limetaka kusitishiwa kwa utoaji wa ‘laini’ mpya za simu.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, kusitishwa huko kwa intaneti kutaanza leo Jumanne (Januari 13, 2026) hadi pale itakapotoka amri ya kurejea.
Hata hivyo, wakosoaji wa Rais Museveni wanaitafsiri hatua hiyo kuwa ni mwendelezo wa utawala wake kuminya uhuru wa kutoa maoni kwa kuzuia wananchi kujadili masuala yanayohusu Uchaguzi Mkuu.
Ikumbukwe, katika Uchaguzi Mkuu huo, Rais Museveni anawania muhula wake wa saba madarakani tangu alipoanza kuiongoza Uganda mwaka 1986.
Kama haijasahaulika, Serikali yake ikichukua hatua hiyo ya kuzima intaneti katika Uchaguzi uliopita wa mwaka 2021. Agizo hilo lilidumu kwa siku 100.


