10.7 C
New York

Carrick, Solskjaer nani apewe jahazi United?

Published:

MANCHESTER, Uingereza

KATI ya malejendari hao wa Manchester United, nani anafaa kupewa mikoba ya kuinoa timu hiyo hadi mwishoni mwa msimu huu?

Michael Carrick, kama ilivyo kwa Ole Gunnar Solskjaer, anapewa nafasi kubwa, kila mmoja akionekana ana sifa kutokana na kazi nzuri aliyofanya.

Awali, Carrick alikuwa akitajwa zaidi, lakini ghafla jina la Solskjaer limeibuka katika mazungumzo ya mabosi wa Old Trafford.

Kwa sasa, kikosi cha Man United kinanolewa na mchezaji mwingine wa zamani, Darren Fletcher, ambaye amekiongoza katika michezo miwili; sare ya mabao 2-2 dhidi ya Burnley na kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Brighton.

Mwandishi wa habari za michezo nchini Italia, Fabrizio Romano, amedai kuwa Carrick ndiye anayepewa kipaumbele na mabosi wa Man United.

Akaeleza kuwa kiungo huyo wa zamani ameshakutana na mabosi na kufanyiwa usahili wa kibarua hicho cha kuinoa Man United hadi mwishoni mwa msimu huu.

Carrick alikuwa kocha wa muda wa Man United baada ya Solskjaer kufutwa kazi Novemba, 2021. Katika mechi tatu alizokaa kwenye benchi, alishinda mbili na kutoa sare moja.

Muingereza huyo aliondoka Old Trafford na kutua Middlesbrough aliyoinoa kuanzia Oktoba, 2022 hadi Juni, 2025. Katika mechi 136, Carrick alishinda 63 na kufungwa 24.

Msimu wake wa pili klabuni hapo ulikuwa wa mafanikio zaidi, ambapo Middlesbrough ilifika nusu fainali ya Kombe la Ligi (EFL).

Mwaka 2024, alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu lakini alifungashiwa virago baada ya timu hiyo kumaliza msimu wa Championship ikiwa nafasi ya 10 katika msimamo.

Kwa upande wake, Solskjaer raia wa Norway alikuwa kocha wa Man United kuanzia mwaka 2018 hadi 2021. Alifutwa kazi akiwa ameshinda asilimia 54 ya mechi 168 alizokaa kwenye benchi.

Man United itarejea dimbani Jumamosi ya wiki hii kwa kuikaribisha Manchester City, kabla ya kusafiri hadi Kaskazini mwa London kuifuata Arsenal.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img