22 C
New York

Nini kiko nyuma ya pazia maandamano Iran?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

YAMEKUWAPO maandamano makubwa nchini Iran, ikikumbukwa kuwa yalianza Desemba 28, 2025 mjini Tehran. Wachambuzi wa siasa wanayataja maandamano hayo kuwa makubwa zaidi tangu yale ya ‘Women, Life, Freedom’ yaliyoitikisa Serikali mwaka 2022.

Katika kukabiliana na presha, video zilizosambaa mitandaoni zinawaonesha polisi wakitumia mabomu ya machozi na risasi za plastiki kuwatuliza waandamanaji. Kwa mujibu wa kile wanachosema waandamanaji hao, wanataka Serikali iliyoko madaakani kuachia ngazi. Nini chanzo cha hasira za wananchi dhidi yake?

Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Central Florida nchini Marekani, Kasra Qaredaghi, anafichua kuwa chazo cha maandamano hayo ni hali ya kiuchumi.

“Katika mazingira ya kupanda kwa gharama za maisha, lakini bado kipato na uhakika wa kazi haupo. Ugumu wa maisha unachangia,” anasema Qaredaghi.

Kushuka kwa thamani ya fedha ya Iran (Rial), hivyo kusababisha mfumuko wa bei kufikia zaidi ya asilimia 42 na kusababisha kupanda kwa gharama za bei ya bidhaa.

“Hali mbaya hii ya kiuchumi inasababisha watu kupoteza imani kwa Serikali, wakiamini imeshindwa kudhibiti mfumuko wa bei na kurekebisha changamoto zilizojitokeza,” anasisitiza Qaredaghi.

Wakati huo huo, mbali ya kashfa za rushwa katika taasisi za umma, hasira za wananchi zinatokana na ushiriki wa Serikali katika migogoro ya nje ya nchi, huku wao wakiendelea kuteswa na ugumu wa maisha.

Mathalan, wengi wao hawavutiwi na sapoti kubwa ya Serikali ya Iran kwa wapiganaji wa Hamas (Palestina) na Hezbollah (Lebanon).

Kwa upande mwingine, Adnan Hassanpour ambaye ni mwandishi wa habari na mwanaharakati wa Iran anayeishi uhamishoni mjini Paris, anasema:

“Kutokuridhishwa na utawala kumefikia kiwango cha juu katika sekta zote. Kwa mujibu wa tafiti, asilimia 92 ya wananchi hawaridhishwi na mambo yanavyokwenda.”

Mwisho, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amechukua hatua kadhaa kukabiliana na presha kubwa inayotokana na maandamano yanayoendelea.

Achilia mbali kumng’oa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, pia ameahidi kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa maandamano hayo makubwa.

Naye msaidizi wake, Mohammad Jafar Ghaempanah, si tu ameomba radhi kwa mfumuko wa bei, bali pia amesema vikwazo vya kiuchumi walivyowekewa na mataifa ya Magharibi ndivyo vilivyochangia changamoto hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img