Na mwandishi wetu, Gazetini
JENERALI wa jeshi, Mamady Doumbouya, ametangazwa kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini Guinea.
Kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya Uchaguzi, Doumbouya ameibuka kidedea baada ya kukusanya asilimia 86.7 ya kura zilizopigwa.
Aliyeshika nafasi ya pili ni Abdoulaye Yero Balde wa Chama cha Democratic Front of Guinea, ambaye hata hivyo ameambulia asilimia 6.6 tu ya kura zote.
Katika nafasi ya tatu, ni Faya Lansana Millimono wa Liberal Bloc, ambaye amepata asilimia 2 pekee.
Kwa matokeo hao, Doumbouya ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021, ataiongoza Guinea kwa kipindi cha miaka saba.
Hata hivyo, asasi za kiraia hazijaridhishwa na matokeo hayo, na badala yake zimeutaja Uchaguzi huo kutawaliwa na sarakasi nyingi.
Mbali ya baadhi ya wagombea wa upinzani wenye ushawishi kuzuiwa kugombea kiti cha urais, pia mitandao ya kijamii ya TikTok, YouTube na Facebook haikuwa ikifanya kazi nchini Guinea wakati wa kuhesabu kura.


