18 C
New York

Watu 13 wafariki, zaidi ya 90 wajeruhiwa baada ya treni kuacha njia Mexico

Published:

OAXACA, Mexico

TAKRIBAN watu 13 wamefariki dunia na wengine karibu 100 kujeruhiwa baada ya treni ya abiria kuacha njia ya reli katika jimbo la Oaxaca, kusini-magharibi mwa Mexico, kwa mujibu wa jeshi la wanamaji la nchi hiyo.

Treni hiyo ilikuwa ikisafiri kati ya Ghuba ya Mexico na Bahari ya Pasifiki, ikiwa imebeba abiria 241 pamoja na wafanyakazi tisa. Jeshi la wanamaji limesema jumla ya watu 98 walijeruhiwa katika ajali hiyo, huku 36 kati yao wakilazwa hospitalini kwa matibabu zaidi.

Ajali hiyo ilitokea treni ilipokuwa ikizunguka kona karibu na mji wa Nizanda, ambapo iliondoka kwenye reli kwa sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.

Mwanasheria Mkuu wa Mexico amethibitisha kuwa uchunguzi wa kina umeanzishwa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo. Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum, amesema kuwa kati ya waliojeruhiwa, watu watano wako katika hali mbaya.

Picha na video kutoka eneo la tukio zinaonyesha vikosi vya uokoaji vikisaidiwa na maafisa wa dharura wakiwatoa abiria ndani ya treni na kuwapatia huduma za awali.

Safari za treni hiyo zinaendeshwa na jeshi la wanamaji la Mexico, ambalo pia limeshiriki kikamilifu katika operesheni ya uokoaji na kutoa msaada kwa waathirika wa ajali hiyo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img