18 C
New York

Jinsi Putin alivyowadhibiti Oligarchs wa Urusi

Published:

MOSCOW, Urusi

Idadi ya mabilionea nchini Urusi imeongezeka kwa kasi na kufikia kiwango cha juu zaidi, hususan katika kipindi cha vita vya Ukraine. Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo la utajiri, katika miaka 25 ya utawala wa Rais Vladimir Putin, matajiri wakubwa wa Urusi-wanaojulikana kama oligarchs -wamepoteza kwa kiasi kikubwa ushawishi wao wa kisiasa.

Kwa Putin, hali hii ni ushindi wa kimkakati. Vikwazo vya Magharibi vilivyolenga matajiri hao vimeshindwa kuwageuza kuwa wapinzani wake wa kisiasa. Badala yake, kupitia sera kali na za kulazimisha, serikali ya Kremlin imewafanya wengi wao kuwa wafuasi wa kimya au waliokubali hali kwa hofu.

Mfanyabiashara bilionea wa zamani, Oleg Tinkov, anatoa mfano halisi wa namna mfumo huo unavyofanya kazi. Tinkov, aliyekuwa mwanzilishi wa Benki ya Tinkoff-iliyokuwa benki ya pili kwa ukubwa nchini Urusi-alikumbwa na mkono mzito wa dola baada ya kuikosoa waziwazi vita vya Ukraine.

Siku moja tu baada ya kuwaita wanaoendeleza vita hivyo “vichaa” kupitia mtandao wa Instagram, Kremlin iliwasiliana na wakurugenzi wa benki yake. Ujumbe ulikuwa wazi: benki hiyo ingetwaliwa na serikali endapo isingekatisha uhusiano wake na mwanzilishi wake.

“Sikuwa huru kujadili bei,” Tinkov alinukuliwa na The New York Times. “Nilikuwa kama mateka. Unachopewa ndicho unachokichukua.”

Ndani ya wiki moja, kampuni inayohusishwa na Vladimir Potanin—mfanyabiashara wa tano kwa utajiri nchini Urusi na muuzaji mkubwa wa nickel inayotumika katika injini za ndege za kivita—ilitangaza kuinunua Benki ya Tinkoff. Kwa mujibu wa Tinkov, benki hiyo iliuzwa kwa asilimia tatu tu ya thamani yake halisi.

Hatimaye, Tinkov alipoteza karibu dola bilioni tisa za Kimarekani ($9bn) za utajiri wake na kulazimika kuondoka Urusi. Tukio hilo linaonyesha mabadiliko makubwa ya mizani ya nguvu, ukilinganisha na kipindi cha kabla ya Putin kuingia madarakani.

Baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Kisovieti, Warusi wachache walijipatia utajiri mkubwa kwa kumiliki makampuni yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali, wakitumia mianya ya ubepari changa wa taifa hilo. Utajiri huo uliwapa ushawishi mkubwa wa kisiasa, kiasi cha kuathiri mwelekeo wa uongozi wa juu wa nchi.

Oligarch aliyekuwa na nguvu zaidi wakati huo, Boris Berezovsky, aliwahi kudai kuwa alimsaidia Vladimir Putin kuingia madarakani mwaka 2000. Miaka kadhaa baadaye, alikuja kuomba msamaha hadharani kwa hatua hiyo.

“Sikuona mapema udhalimu wake-mtu ambaye angebana uhuru na kurudisha nyuma maendeleo ya Urusi,” Berezovsky aliandika mwaka 2012.

Ingawa huenda alizidisha nafasi yake katika kumpandisha Putin madarakani, hakuna shaka kwamba oligarchs wa Urusi waliwahi kuwa na uwezo mkubwa wa kushinikiza mabadiliko ya kisiasa.

Zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuandika barua hiyo ya majuto, Berezovsky alipatikana amekufa katika mazingira ya kutatanisha akiwa uhamishoni nchini Uingereza. Kufikia wakati huo, zama za ushawishi wa oligarchs nchini Urusi zilikuwa zimefikia ukingoni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img