DHAKA, Bangladesh
VURUGU kubwa zimeibuka nchini Bangladesh baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa mandamano ya mwaka jana yaliyomng’oa madarakani Waziri Mkuu, Sheikh Hasina.
Sharif Osman Hadi alipigwa risasi na watu waliokuwa wameficha nyuso zao kwa kinyago wakati akitoka msikitini mjini Dhaka wiki iliyopita.
Taarifa zinaeleza kuwa Osman Hadi amefariki Desemba 18, 2025, akiwa kwenye matibabu katika moja ya hospitali nchini Singapore.
Tukio la kupigwa risasi limekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya mamlaka za Bangladesh kutangaza tarehe ya Uchaguzi wake wa kwanza tangu mapinduzi yaliyomtoa Hasina.
Ifahamike kuwa Hadi alishatangaza nia ya kugombea kiti cha Waziri Mkuu kilichoachwa wazi na Hasina wakati wa maandamano ya mwaka jana.
Baada ya taarifa za kifo cha Hadi, zimezuka vurugu zilizosababishwa na maandano ya vijana waliokusanyika mjini Dhaka.
Katika vurugu hizo, waandamanaji wameharibu baadhi ya ofisi, ikiwamo kuchoma moto makao makuu ya magazeti maarufu ya Daily Star na Prothom Ali.


