CAIRO, Misri
FAINALI za Mataifa ya Afrika za mwaka huu (AFCON 2025) zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 21, mwaka huu. Zitafanyika nchini Morocco.
Kati ya timu 24 zitakazoshiriki, zipo zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo, zikiwamo Misri, Ghana, Nigeria na mabingwa watetezi, Ivory Coast.
Hata hivyo, zipo baadhi ya timu zisizozungumziwa sana, lakini zinaweza kuwashangaza wengi katika michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Ni kama ilivyokuwa katika fainali za mwaka 2012, ambapo Zambia ‘Chipolopolo’ haikuwa ikipewa nafasi lakini iliwashangaza wengi baada ya kutwaa ubingwa.
Afrika Kusini
‘Bafana Bafana’ ni mabingwa mara moja wa fainali hizo. Walitwaa ubingwa wao pekee wakiwa wenyeji wakati wa fainali za mwaka 1996.
Msimu uliopita wa AFCON, walifika nusu fainali na kushika nafasi ya tatu. Pia, Afrika Kusini imeshafuzu fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.
DRC
Historia ya AFCON inaitambua kuwa hao ni mabingwa mara mbili, ingawa wakati huo nchi hiyo ilifahamika kwa majina ya Congo-Kinshasa (1968) na Zaire (1974).

Kwa sasa, DRC ina kikosi chenye wachezaji wakubwa, wakiwamo Noah Sadiki, Aaron Wan-Bissaka, Axel Tuanzebe, Samuel Essende na Cedric Bakambu. Pia, wanaye kocha mzoefu raia wa Ufaransa, Sebastien Desabre.
Gabon
Walikosa pointi moja pekee kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani. Ni katika kundi walilokuwa na Ivory Coast iliyokata tiketi.
Gabon, ambayo nahodha wake ni straika wa zamani wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, haijawahi kuvuka robo fainali ya AFCON lakini huenda ikafanya maajabu msimu huu.
Burkina Faso
Wana kikosi chenye uwezo wa kuitikisa AFCON. Burkina Faso ya Bertrand Traore, Dango Ouattara, Edmond Tapsoba na mastaa wengine wanaokipiga barani Ulaya.
Mafanikio yao makubwa zaidi kwenye AFCON ni kufika fainali mwaka 2013, ingawa walikosa ubingwa baada ya kufungwa na Nigeria. Msimu uliopita, waliishia hatua ya 16 Bora wakiondoshwa na Mali.


