Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura kuhakikisha ukamataji wa watuhumiwa unafanywa kwa kufuata taratibu za kisheria na staha.
Pia amezuia Polisi kufanya ukamataji wakiwa wamevaa vifunika uso ( kininja) bila sare na wakiwa na silaha kubwa na ufanyike mchana kwa taarifa za wazi .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Simbachawene amesema ukamataji usifuata sheria unazua hofu kwa familia za watu wanaokamatwa.
“Ukamataji ninaoutaka mimi ni ule wa kisheria, askari anaenda anaripoti kwa mjumbe, mtu anajulikana yupo kazini kwake kwa nini uende kumkamata nyumbani kwake ukiwa umevaa kininja? Tumekubaliana kwamba kuwe na ukamataji wenye staha,” amesema.
Aidha amekosoa tabia ya kukamata watu kwa makosa madogo kama kuposti posti ndogo mitandaoni, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinachochea chuki dhidi ya Polisi wakati Jeshi hilo ndilo linahakikisha usalama wa wananchi
Waziri huyo ametoa angalizo kwa wananchi kutoshiriki kile kinachoelezwa kama maandamano ya amani yasiyo na mipaka wala mwisho yanayohamasishwa mitandaoni na katika maeneo mbalimbali nchini.


