Na mwandishi wetu, Gazetini – DAR
HIVI karibuni, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifuta adhabu ya vikobo shuleni, hivyo kuungana na mataifa mengi duniani yaliyowahi kufikia uamuzi huo.
Ni adhabu ambayo kwa miaka mingi, tangu karne ya 19 na 2020, ilikuwa ikitumika kama njia ya kuwanyoosha wanafunzi wasio na nidhamu au wanaokiuka taratibu wawapo shuleni.
Hata hivyo, tafiti zimeshindwa kuthibitisha kuwa adhabu ya viboko imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwarejesha kwenye mstari wanafunzi hao walioonekana kukengeuka.
Na badala yake, tafiti zimejiridhisha kuwa adhabu hiyo imesababisha madhara ya kimwili, kwa maana ya majeraha, na hata kuathiri saikolojia ya wanafunzi.
Kwa sasa, nchi zaidi ya 120 duniani zimepiga marufuku matumizi ya fimbo shuleni na Finland ni miongoni mwa nchi za kwanza, ikifanya hivyo mwaka 1914, huku China ikifuata nyayo mwaka 1949.
Pia, Australia ilipiga marufuku mwishoni mwa miaka ya 1980, wakati Uingereza iliyofanya hivyo kwa shule za Serikali mwaka 1987, kabla ya kuongeza zile za binafsi mwaka 1998.
Baadhi ya nchi zingine ni Ujerumani [1993], Denmark [1967], Canada [2004], Ugiriki [2005], Colombia [2006], Costa Rica [2008], Argentina [2016], na Ufaransa [2019].


