MUNICH, Ujerumani
STRAIKA wa Bayern Munich, Harry Kane, atakuwa nje ya uwanja kwa miezi michache ijayo baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu [enka] katika mchezo wa jana Novemba 20, 2026, uliomalizika kwa timu yake kutoka sare ya bao 1-1 na Cologne.
Kane aliyetwaa tuzo ya Ballon d’Or mwezi uliopita, alilazimika kutoka uwanjani akiwa amecheza dakika 20 za mwanzo baada ya kuchezewa rafu na beki wa Cologne, Joel Schmied.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na klabu yake, nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 ameumia enka ya mguu wake wa kushoto.
Hadi anakwenda benchi na kumpisha Tom Bischof, Bayern walikuwa nyuma kwa bao 1-0, mfungaji wa Cologne akiwa kinda wa U-21 ya England, Mikey Moore.
Aliyeiokoa Bayern kwa bao la kusawazisha ni Nathaniel Brown, ambaye ilikuwa mechi yake ya kwanza baada ya kukosekana kwa muda mrefu kutokana na majeraha.
Kumpoteza Kane ni pigo kubwa kwa Bayern kwani straika huyo ameshafunga mabao manne na kutoa asisti nane katika mechi 10 za msimu huu wa Bundesliga.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, nyota huyo wa zamani wa Tottenham ameishaifungia Bayern jumla ya mabao manne na asisti tatu katika michezo minne tu waliyocheza.


