10.2 C
New York

Cop31 yafunguliwa, nchi zashinikizwa kutekeleza ahadi za tabianchi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

ZAIDI ya watu 90,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo Antalya, huku ufadhili na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zikitawala majadiliano

Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) ikiwamo Tanzaniam umefunguliwa jijini Antalya, Uturuki, huku zaidi ya watu 90,000 wakitarajiwa kushiriki na shinikizo likiongezeka kwa nchi kutimiza ahadi zao za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo, unaotarajiwa kuhitimishwa Ijumaa, Novemba 20, 2026, unafanyika wakati nchi zinazoendelea zikisisitiza umuhimu wa kupata fedha kwa wakati ili kukabiliana na athari za tabianchi, huku washiriki wakitaka ahadi za kimataifa zitafsiriwe kuwa hatua halisi.

Akifungua mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell, amesema dunia inapaswa kuingia katika hatua mpya ya utekelezaji kwa kuhakikisha malengo ya kimataifa na mipango ya kitaifa ya tabianchi yanageuzwa kuwa vitendo, hususan katika ufadhili wa kukabiliana na athari za tabianchi, nishati jadidifu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

“COP31 lazima uongeze kasi ya kutafuta na kutekeleza suluhisho,” amesema Stiell, akisisitiza umuhimu wa kutimiza ahadi za kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, kuondoa vikwazo vinavyozuia nchi kupata ufadhili uliopo na kuongeza mara tatu uwezo wa uzalishaji wa nishati jadidifu duniani ifikapo mwaka 2030.

Amesema ingawa asilimia 90 ya miradi mikubwa ya nishati jadidifu sasa ina gharama nafuu kuliko miradi ya nishati za kisukuku, maendeleo yaliyofikiwa bado hayatoshi na hayajasambazwa kwa usawa.

Ufadhili na haki vipewe kipaumbele

Rais wa COP31, Murat Kurum wa Uturuki, ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuziba pengo kati ya ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hali halisi zinazokabili jamii zilizo katika hatari zaidi.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuathiri uhakika wa chakula, uhamiaji, upatikanaji wa nishati, uchumi na afya ya binadamu, hivyo sera za tabianchi zinapaswa kuwa sehemu muhimu ya sera za maendeleo.

“Tunafahamu kuwa kuchelewa kuchukua hatua ni moja ya gharama kubwa zaidi katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” ameonya Kurum, akieleza kuwa kuchelewesha uwekezaji katika ustahimilivu na ufadhili wa kukabiliana na athari za tabianchi kunaweza kuongeza maafa na majanga ya kibinadamu siku zijazo.

Amezitaka nchi kuhakikisha lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5 linabaki kuwa mwongozo wa hatua za kukabiliana na tabianchi, huku nchi na jamii zilizo katika hatari zaidi zikipata nafasi kubwa katika majadiliano.

Kurum pia amesisitiza umuhimu wa kubadili ahadi za ufadhili wa tabianchi kuwa uwekezaji halisi, akirejelea makubaliano ya Baku ya kutoa angalau dola bilioni 300 za Marekani kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ifikapo mwaka 2035, sambamba na juhudi za kuongeza ufadhili kutoka sekta za umma na binafsi hadi angalau dola trilioni 1.3 kwa mwaka.

Australia yataka makubaliano yafikiwe mapema

Waziri wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati wa Australia na Rais wa Mazungumzo ya COP31, Chris Bowen, amesema mabadiliko ya tabianchi tayari ni hali halisi inayowaathiri mabilioni ya watu duniani, hivyo nchi zinapaswa kuharakisha hatua za kukabiliana nayo badala ya kuendelea kutoa ahadi bila utekelezaji.

Akitoa mifano ya athari hizo, ametaja kuyeyuka kwa barafu katika milima ya Nepal, vifo vinavyotokana na joto kali barani Ulaya na kuongezeka kwa nguvu kwa hali ya hewa ya El Niño.

“Mabadiliko ya tabianchi yapo sasa. Si utabiri wala makisio. Ni hali halisi inayowakabili mabilioni ya watu,” amesema Bowen, akizitaka nchi kuharakisha hatua za kukabiliana na tabianchi, kurahisisha upatikanaji wa fedha na kuimarisha ustahimilivu wa jamii na uchumi.

Ametoa pia wito wa kuongeza uwekezaji katika nishati jadidifu, mifumo ya kisasa ya usambazaji umeme, teknolojia za kuhifadhi nishati na matumizi ya umeme katika sekta mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa nchi kutimiza ahadi zao za ufadhili wa tabianchi.

Katika hatua nyingine, Australia imetaka nchi zianze kujenga makubaliano ya kisiasa tangu mwanzo wa mkutano badala ya kusubiri siku za mwisho, ili kuongeza nafasi ya kufikia maamuzi kwa wakati.

Chakula, kilimo na afya vyapewa uzito

Mkutano huo pia unaangazia athari za mabadiliko ya tabianchi katika maisha ya watu, hususan katika sekta za chakula, kilimo na afya.

Kupitia siku maalumu ya kujadili masuala hayo, washiriki wanatarajia kujadili hatari zinazoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na suluhisho za vitendo zinazoweza kusaidia kulinda maisha na shughuli za kiuchumi za jamii.

Kwa ujumla, mkutano huo unatarajiwa kujadili zaidi ya ajenda 160 na masuala 60 ya msingi, yakiwemo kukabiliana na athari za tabianchi, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, mpito wa haki kuelekea uchumi usiotegemea nishati chafuzi na ufadhili wa tabianchi.

Karibu nchi 200 zinashiriki mkutano huo katika pwani ya Mediterania nchini Uturuki, huku wajumbe wakikabiliwa na changamoto ya kugeuza ahadi na matamko ya kimataifa kuwa maamuzi na hatua madhubuti.

Hali hiyo inakuja wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kuathiri jamii mbalimbali duniani, huku matarajio ya kuongezeka kwa nguvu kwa hali ya hewa ya El Niño yakiongeza umuhimu wa hatua za kuimarisha ustahimilivu na kulinda maisha ya watu.

Related articles

Recent articles