18.8 C
New York

Mashabiki United walipomshangilia straika aliyewatungua ‘hat trick’

Published:

MANCHESTER, Uingereza

STRAIKA mwenyewe ni huyu; Ronaldo Nazario, ambaye ametimiza umri wa miaka 50. Mshambuliaji mwenye historia ya kubeba tuzo mbili za Ballons d’Or na Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya Taifa ya Brazil ‘Selecao’.

Kwa mashabiki wa Manchester United, jina la Ronaldo litabaki kwenye kumbukumbu zao kwa kile alichowafanyia usiku mmoja wa Aprili, 2003, wakati alipokutana nao akiwa na kikosi cha Real Madrid.

Ilikuwa ni mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa Old Trafford na Madrid walikwenda ugenini wakiwa tayari wanaongoza kwa ushindi wa 3-1 walioupata katika mechi ya kwanza Santiago Bernabeu.

Man United chini ya Alex Ferguson waliamini ‘wangepindua meza’ wakiwa nyumbani lakini Ronaldo aliipeperusha ndoto yao hiyo baada ya kupachika ‘hat-trick’, hivyo Real Madrid kusonga mbele licha ya kufungwa mabao 4-3. Walibebwa na matokeo ya awali [3-1].

Ronaldo alifunga bao la kwanza katika dakika ya 12 tu ya kipindi cha kwanza na ni mchezo ambao David Beckham alitokea benchi na kufunga mabao mawili, wakati kipa wa United akiwa ni Fabien Barthez.

Tukio kubwa zaidi ni lile la mashabiki wa Man United kujikuta wakisahau maumivu na kunyanyuka kwenye viti vyao ili kumpa heshima Ronaldo wakionesha kuvutiwa na kiwango kizuri alichowaonesha katika mchezo huo.

Licha ya safari yake ya soka la kulipwa barani Ulaya kuandamwa na majeraha ya goti, Ronaldo aliweza kutwaa Ballon d’Or mwaka 1997 na 2002. Aliwahi kupita Barcelona, Inter Milan na Real Madrid.

Related articles

Recent articles