26.5 C
New York

‘Mitandao ya kijamii siyo daktari, chukua tahadhari’

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

UTAFITI uliochapishwa katika Jarida la JAMA unaoonesha kuwa mmoja kati ya watu watano nchini Marekani wanafanya maamuzi ya kinga na tiba kwa kufuata taarifa wanazopata mitandaoni.

Mtaalamu wa afya na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Washington, Dkt. Leana Wen, amesema watu takribani milioni 47 nchini Marekani wanategemea taarifa za mitandaoni kufanya maamuzi juu ya afya zao.

KWANINI MITANDAO?

Kwanini wengi wanakimbilia mitandaoni kupata taarifa hizo za afya? Dkt. Wen anajibu akisema: “Zipo sababu nyingi. Ni njia rahisi, ya haraka, haina gharama na huduma inapatikana muda wowote.

“Baadhi ya majukwaa yana video au michoro rahisi kueleweka … Pia, watu wanaweza kusikia ushuhuda wa wenzao wenye matatizo kama yao. Ni njia rahisi kuliko inavyoelezwa kwenye vitabu au tovuti.

Sababu ya pili anayoitaja Dkt. Wen ni ugumu uliopo katika mifumo rasmi ya utoaji wa huduma za afya. “Kwenda hospitali wakati mwingine inagharimu muda na pia watu wanaondoka wakiwa hawana majibu ya kutosha ya maswali juu ya magonjwa yao,” anasema.

“Hapo ndipo wagonjwa wanapoamua kugeukia mitandao ya kijamii ili kupata uelewa zaidi, kusikia kutoka kwa wenzao, au kujifunza namna ya kuishi na magonjwa hayo.”

HATARI ILIYOPO

Wasiwasi wa wataalamu wa afya ni kwamba taarifa nyingi za mitandaoni si za kuaminika na zimejaa upotoshaji, hivyo si sahihi kutumika katika suala nyeti la afya.

Wataalamu wanasema changamoto ya taarifa za mitandaoni hazitofautishi ushauri wa kitaalamu na maoni binafsi, jambo linaloweza kuzalisha upotoshaji mkubwa wa kinga na tiba.

Dkt. Wen anasema hata akili-unde (Artificial Intelligence) haijaimarika kiasi cha kuaminika katika kila taarifa inayotoa kuhusu kinga na tiba za magonjwa.

“Mifumo ya AI haijawa timamu vya kutosha kutoa majibu sahihi ya kiafya. Hivyo, hakikisha unamshirikisha mtaalamu wa afya katika kila taarifa ya mtandaoni,” anasema Dkt. Wen.

Wakati huo huo, Dkt. Wen anasema baadhi ya watengeneza maudhui wa mitandaoni wanaweza kulipwa fedha ili kutoa taarifa zisizo sahihi juu ya dawa au vipimo.

FANYA HAYA UBAKI SALAMA

Hata hivyo, wataalamu wanakubaliana kuwa licha ya wasiwasi uliopo, yapo majukwaa sahihi yanayoweza kuaminika kwa taarifa za afya huko mitandaoni.

“Ndiyo. Wapo wauguzi, wanasayansi, mashirika ya afya, hospitali na taasisi zinazotoa taarifa sahihi, zenye ushahidi wa kitaalamu kwenye majukwaa mbalimbali ya mitandaoni.

“Swali la kwanza unalopaswa kujiuliza ni nani anayetoa taarifa? Ni muuguzi, mwanasayansi, chuo cha afya, au shirika la afya la serikali?

“Pili, hata kama ni chanzo cha kuaminika, taarifa yake inaegemea katika ushahidi wa kitaalamu na si maoni binafsi?

“Tatu, kuwa makini endapo utatakiwa kulipia ushauri, kinga au tiba. Pia, kuwa makini ikiwa taarifa zinakuahidi kupona haraka.

“Nne, thibitisha taarifa kabla ya kuzifanyia kazi. Fanya utafiti katika taasisi zingine zinazoaminika, mathalan Shirika la Afya la Kimataifa (WHO).

Related articles

Recent articles