BEIJING, China
KATIKA nchi nyingi duniani, maeneo ya mijini yameonekana kuwa ndiyo fursa ya kukimbilia, hasa kwa vijana wenye ndoto za kuishi maisha mazuri.
Kwa Beijing, Mji Mkuu wa China, mambo yamekuwa tofauti katika miaka ya hivi karibuni. Vijana wanapakimbia na kuhamia vijijini au kwenye miji midogo.
Kundi hilo la vijana linahusisha wahitimu wa vyuo vikuu, wajasiriamali na wahamiaji, ambao kwa sasa wanayaona maeneo ya vijijini kama kama kitovu cha ustawi wa maisha yao. Kwanini?
Wang Lei, kijana mwenye umri wa miaka 29, ni miongoni mwao. Alizaliwa katika Jimbo la Hebei, kisha kuhamia Beijing akiwa na miaka 20.
Kama ilivyo kwa vijana wengi, alipofika Beijing na kukuta Mji umechangamka kwa miundombinu, alipata picha ya kutimia kwa ndoto yake ya maisha bora.
Baada ya miaka sita ya kuishi Beijing, Lei sasa anakutana na picha tofauti na aliyokuwa nayo wakati anaingia katika Jiji hilo.
Idadi ya watu milioni 22 imeminya kwa kiasi kikubwa nafasi za ajira na kuzifanyia ziwe chache na za kupigania.
Gharama za vyakula, kodi na huduma zingine ziko juu, hali iliyosababisha ugumu wa maisha kwa walio wengi.
“Watu wengi, wakiwamo marafiki zangu, wanakabiliwa na msongo wa mawazo kama mimi. Mishahara wanayopata haiendani na gharama za maisha.
“Ukiweka na mahusiano, kodi na safari za hapa na pale, ndiyo kabisa. Pesa haitoshi,” anasema Lei.
Kuthibisha Beijing ilivyo ngumu kwa vijana, imekuwapo ‘hashtag’ ya ‘Kurotoka Beijing’ inayosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii ya China.
Mtazamo wa vijana ni kwamba Beijing siyo tena sehemu salama ya kupigania ndoto zao, hivyo ni lazima waondoke na kurudi vijijini au kwenda kuanza maisha kwenye miji midogo.
Hoja yao ni kwamba pesa kidogo waliyopata Beijing inaweza kuwapa maendeleo na kuishi vizuri wakiwa nje ya Jiji hilo.
“Kwa pesa hii ninayopata, naweza kuishi maisha mazuri katika maeneo mengine. Nimekuja kugundua kuwa watu walioondoka Beijing kwa sasa wana furaha kuliko mimi.
“Wamepunguza presha na msongo wa mawazo. Wana maisha ya uhuru kuliko nilivyo mimi,” amesema Lei.
Hata hivyo, anakiri kuwa licha ya vijana wengi kutamani kuondoka Beijing, baadhi yao wanasita kufanya uamuzi huo wakihisi watachekwa kwa kushindwa ‘kukomaa’ mjini.
Hata hivyo, kwa Lei, mtazamo umebadilika na sasa anaamini maisha siyo kuishi mjini, bali kokote kunakompa fursa ya kupiga hatua, hasa kiuchumi.
Kwako msomaji wa makala haya; mazingira unayoishi, bila kujali ni mjini au kijijini, yana mchango gani katika kukupa maendeleo na furaha ya maisha?


