23.1 C
New York

Matajiri wa Katoro walivyolisimamisha Jiji

Published:

Na Hassan Mwasha

VIDEO iliyosambaa mitandaoni ikiwaonesha wafanyabishara matajiri kutoka wilayani Katoro mkoani Geita wakimwaga pesa katika sherehe ‘ime-trend’ hivi karibuni kwenye tasnia ya burudani hapa nchini.

Ni ‘send-off’ ya msichana aitwaye Monalisa, ambaye ni binti wa mmoja ya matajiri hao anayefahamika kwa jina Sylvester Buyamba ‘GSM wa Katoro’.

Katika video hiyo, vibopa hao wanaonekana wakitunza pesa nyingi, huku Monalisa akiwekewa kwenye akaunti yake ya benki zaidi ya Shilingi bilioni moja.

Tangu ilipoibuka video hiyo, watengeneza maudhui ya mitandaoni wamezua mjadala mkubwa, wakivutana juu ya ni wapi kuna matajiri wakubwa kati ya Dar es Salaam na mikoani.

Baadhi yao wameibuka na kudai kuwa wafanyabiashara wenye pesa nyingi wako mikoani, huku wengine wakiitaja Dar kuwa ndiyo inayoongoza.

Kwa upande wake, mtengeneza maudhui maarufu, Mwijaku, alibeza kile kilichofanyika Katoro, akisistiza kuwa Dar ndiyo sehemu yenye matajiri wengi na si mikoani.

“Mtu kama mimi, siwezi kusema Katoro kuna matajiri. Miaka 10 iliyopita, Waarabu walikuwa wanafanya sherehe, kuwaita wasanii sebuleni kwao na kuwatunza mahela (fedha) …”

Kauli hiyo ilimuibua mtengeza maudhui maarufu kutoka jijini Mwanza, Poul Brand, akisema Dar hakuna matajiri wa kuwazidi wa mikoani.

Alienda mbali zaidi na kusema wanaojiita matajiri wa Dar hawamuru hata kuishi maeneo ghali, ikiwamo Masaki, na badala yake ni wafanyabiashara wa mikoani na raia wa kigeni tu ndiyo wanaoishi huko.

Amesema: “Unafikiri hatujui, Masaki hiyo ni ya Wachina na matajiri zangu wa Kanda ya Ziwa wamenunua majengo mengi sana. Wamenunua majengo mengi huko Masaki, Kigamboni. Hiyo Sinza yote …”

Kwa upande wake, mtengeza maudhui mwingine, Chief GodLove, anaungana na Paul Brand akisema wafanyabishara wa mikoani wana ‘sasampa’ kuliko wenzao wa Dar.

Katika video aliyojirekodi, Chief amesema: “Mpaka sasa hivi gemu linavyokwenda, watu wa mjini (Dar) ni sifuri, watu wa Katoro (mikoani) ni 100.

“Watu wa kijijini hawataki historia, kwamba sijui tajiri fulani ana kiwanja Mbweni, sijui tajiri fulani anamiliki sijui nini. Hawataki hizo.

“Watu wa kijijini wanataka hivi; wakiweka bilioni nne mezani, na wewe nenda kalete bilioni 10 uweke mezani. Wale (wa Katoro) bilioni moja wametunza, na nyinyi watu wa Dar mnatakiwa bilioni tano mkatunze …”

Aidha, maoni yake hayo yanapishana kwa mbali na anachoamini mtengeneza maudhui mwingine, Doto Magari, ambaye kwa mtazamo wake Dar ndiyo sehemu pekee nchi hii yenye matajiri.

Alisema: “Na nyie watu wa Nyamongo, huko Musoma, Geita, sijui wapi huko, Mwanza, mnatuchosha. Kwanini mnapenda kujisifia matajiri wako huko?

“Huko sasa kuna tajiri? Musoma, Geita, Mwanza. Huko kuna wafanyabishara, wawekezaji, watu wa kushinda kwenye mashimo kama nyoka …”

Wakati huo huo, kauli yake hiyo imejibiwa na mchambuzi wa muziki, Meneja Ding’ano, aliyefichua kuwa Ali Kiba alilipwa zaidi ya Shilingi milioni 300 kutumbuiza.

Ding’ano anasema: “Halafu Doto Magari anakwambia tajiri anakaaje Kanda ya Ziwa au mikoani. Nataka nimtolee mfano, tajiri yake mkubwa anaitwa Oliva, ndiye tajiri wa Kusini. Anakaa wapi?”

Mwisho, mjadala ni mzito na bado unaacha swali; je, ni kweli Dar inaizidi mikoa mingine kwa kuwa na wafanyabiashara wenye pesa ndefu?

Related articles

Recent articles