LONDON, Uingereza
MSIMU wa 2025-26 haukuwa mzuri kwao. Chelsea walimaliza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England wakiwa nafasi ya 10 kwenye msimamo. Hawatoshiriki michuano ya Ulaya msimu ujao.
Kocha mpya ni Xabi Alonso na tayari ameshaanza mikakati ya usajili ili kuhakikisha msimu ujao Blues wanakuwa kwenye ubora wao wa misimu kadhaa iliyopita.
Ripoti zinaeleza kuwa Marc Cucurella na Enzo Fernandez wako njiani kuondoka Stamford Bridge. Ni kama ilivyo kwa Jamie Gittens, Alejandro Garnacho na Liam Delap.
Katika usajili uliofanyika hadi sasa, Emanuel Emegha ametua akitokea Strasbourg, klabu inayomilikiwa na mabosi wa Blues huko Ufaransa.
Wakati huo huo, ripoti kutoka Ufaransa zinaeleza kuwa mchezaji mwenzake kutoka katika klabu hiyo, Valentin Barco, naye atamfuata Stamford Bridge.
Katika hatua nyingine, zipo tetetesi kuwa Blues wanaangalia uwezekano wa kumrejesha straika wake raia wa Senegal anayecheza Bayern Munich, Nicolas Jackson.


