PARIS, Ufaransa
MWAKA 2011, matajiri wa kampuni ya Qatar Sports Investments ya Qatar walikuwa mezani na mabosi wa klabu ya kawaida tu, PSG. Matajiri wa Kiarabu walitaka kuinunua.
Wakati huo, PSG ilitoka kumaliza msimu wa Ligue 1 ikiwa ya 13 kwenye msimamo. Chini ya Mwenyekiti wa QSI, Nasser Al-Khelaifi, hakusita. Akaweka pesa mezani na kuinunua PSG.
Matajiri wa Qatar wakaanza na PSG ambayo haikuwa na mastaa, mfumo bora wa uendeshaji, wala falsafa ya uchezaji ndani ya uwanja.
Wachezaji pekee walioonekana kuwa tofauti na wengine kikosini ni Ronaldinho, Pauleta, Ludovic Giuly na Claude Makelele, ambao hata hivyo hawakuwa wakivuma katika soka la Ulaya.
Ilipofika mwaka 2016, baada ya msoto wa muda mrefu katika ndoto ya kutawala soka la Ulaya, tajiri Al-Khelaifi alifanya uamuzi mgumu. Matumizi ya fedha nyingi katika soko la usajili.
Badaye, walishuhudiwa Zlatan Ibrahimovic, Marco Verratti, Sergio Ramos, Neymar, Kylian Mbappe na Lionel Messi wakitua kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kuipa PSG heshima katika michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa.
Katika usajili wa mastaa, wakati mwingine mabosi wa PSG walilazimika kukubali baadhi ya masharti magumu. Mbappe alijiunga nao akiwa na umri wa miaka 18 kwa sharti la kucheza kikosi cha kwanza.
Usajili wa Neymar nao ulikuwa na sharti lake. Kwamba Kuna baadhi ya mechi za ugenini ataamua kwenda au kubaki nyumbani.
Wakati huo, Al-Khelaifi na wenzake walikubali yote ili tu kutimiza kile walichokiota wakati wanatoa fedha kuinunua PSG mwaka 2011.
Kinyume chake, uwepo wa mastaa hao bado haukuisaidia timu kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa. Na badala yake, vita ya kila staa kutaka kuwa juu ya wengine ikaanza kukitafuta kikosi.
Kama itakumbukwa, Neymar na Mbappe waliingia kwenye mgogoro mkubwa wa kugombea nani apige penalti iliyotokea katika moja ya mechi za PSG..
Julai, 2023, ni kama matajiri wa PSG waliamua kuanza upya baada ya kuamua kumpa ajira kocha wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania, Luis Enrique.
Huo ukawa mwisho wa kutegemea mastaa, na badala yake kujenga mfumo wa uchezaji wa timu, usajili unaoendana na mahitaji, kisha kusubiri mafanikio.
Tofauti na kutegemea mastaa, Enrique alitengeneza timu yenye wachezaji wengi wenye umri mdogo (wastani wa miaka 23 na siku 363). Makinda sita walipandishwa timu ya wakubwa wakitokea kwenye ‘academy’ yao.
Hatua yake ya kumruhusu Mbappe kuondoka ikionesha wazi mkakati wake wa kurejesha nidhamu kikosini, ambayo kwa miaka mingi ilikosekana kwa wachezaji wa PSG.
Wakati Ousmane Dembele akionekana amekwisha, Enrique akamsajili na kumfanya kuwa kiongozi wa safu yake ya ushambuliaji.
Katika kusisitiza nidhamu, Enrique alimwacha Dembele katika kikosi kilichocheza na Arsenal msimu uliopita, chanzo kikiwa ni kuchelewa mazoezini kwa dakika 10 tu.
Kuanzia hapo, nidhamu kwa wachezaji iliimarika. PSG ikawa timu yenye kadi za njano chache Ulaya. Ikawa ni nadra kwa wachezaji wa timu hiyo kulumbana na waamuzi kama ilivyokuwa awali.
Enrique akasisitiza zaidi umuhimu wa kikosi chake kutokumtegemea mchezaji mmoja katika ufungaji mabao.
Kwake, ni bora kuwa na nyota watano, kila mmoja awe na mabao 10 hadi 12, kuliko kuwa na mmoja anayefunga mabao 40. Ndicho kilichotokea. Msimu huu, PSG ilikuwa na wafungaji 20 tofauti katika mechi zake.
Ndani ya misimu yake miwili jijini Paris, PSG imetwaa mara mbili mfululizo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ametimiza ndoto ya tajiri Al-Khelaifi.


