PARIS, Ufaransa
POLISI nchini Ufaransa wanawashikikia mashabiki zaidi ya 400 wa PSG waliosababisha vurugu katika maeneo mbalimbali nchini humo baada ya timu yao kutwaa taji la Ligi Mabingwa Ulaya usiku wa jana Mei 30, 2026.
PSG walitetea ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Arsenal katika mchezo wa fainali uliochezwa mjini Budapest, Hungary.
Baada ya mchezo kumalizika, mashabiki wa PSG nchini Ufaransa walijikuta wakizidiwa na furaha na kusababisha vurugu zilizoathiri huduma za usafiri jijini Paris.
Baadhi ya matukio yaliyonaswa na kusambaa kwenye mitandao ni mashabiki hao kuwasha moto na kuchoma vitu, zikiwamo baiskeli.
Katika kutuliza vurugu hizo, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki, ikielezwa pia wapo kadhaa waliojeruhiwa.


