LONDON, Uingereza
AKIWA na umri wa miaka 16, bado David Raya hakuwa akifahamika katika ulimwengu wa soka. Alikuwa kipa asiye na nafasi ya kuanza hata kwenye timu za vijana za klabu ya Cornella ya Daraja la Tatu mjini Barcelona, Hispania.
Mwaka 2012, alihamia kwenye ‘academy’ ya Blackburn Rovers ya Uingereza, kama sehemu ya utaratibu wa klabu hizo kubadilishana makinda.
Miaka miwili baadaye, aliondoka ili kupata timu itakayompa nafasi ya kucheza na ilishangaza wengi alipokataa ofa nyingi na kutua kwa mkopo Southport ya Ligi Daraja la Tano nchini Uingereza.
Akiwa na kiu ya kutimiza ndoto, Mhispania huyo alikuwa na utaratibu uliowashangaza wengi. Siku ambazo Southport walipumzika, alikwenda kufanya mazoezi na Blackburn. Hakuwa na muda wa kupoteza.
Mwaka 2019, Raya alisajiliwa na Brentford kwa ada ndogo tu ya Pauni milioni 3, kabla ya Arsenal kumchukua kwa mkopo, kisha kumsajili moja kwa moja kwa Pauni milioni 27.
Ikiwa ni miaka mitano tangu Arsenal walipomsajili, Raya wa sasa ni mkubwa zaidi. Si tu ametimiza ndoto zake, bali pia uwezo wake langoni umeipa Arsenal taji la kwanza la Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kulikosa kwa miaka 22.
Kwa ufupi, ameipa mafanikio Arsenal, pia naye akimaliza msimu wa 2025-26 wa EPL akiwa ndiye Kipa Bora wa Mwaka. Nyota iliyotoka mchangani na kuweka alama soka la Ulaya. Huyo ndiye Raya.


