PRETORIA, Afrika Kusini
ZIKIWA ni siku chache tu zimepita tangu kocha wa zamani wa Yanga, Cedric Kaze, afukuzwe Kaizer Chiefs, ameanza mazungumzo na Sekhukhune United inayoshiriki pia Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Licha ya kugoma kutaja jina la klabu, Kaze amekiri kuwapo kwa mazungumzo. “Kuna mazungumzo yameendelea.
“Kama yatakwenda vizuri, nitachukua kibarua kwa sababu naijua Ligi, nawajua wachezaji na mfumo mzima wa soka la hapa,” amesema.
Kaizer Chiefs ilimfungashia virago kocha huyo raia wa Burundi baada ya kumaliza msimu wa 2025-26 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi.
Kaze alijiunga na timu hiyo akiwa msaidizi wa Nasreddine Nabi aliyewahi pia kuinoa Yanga, kabla ya kocha huyo raia wa Tunisia kuondoka kabla ya msimu kuisha.
Baada ya kuondoka, Kaze alipewa kijiti cha kuliongoza benchi la ufundi akisaidia na Khalil Ben Youssef, ambaye pia aliwahi kupita Yanga akiwa msaidizi wa Nabi.


