LONDON, Uingereza
BEKI wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, ameitabiria ushindi PSG katika fainali yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Washika Bunduki wa London, Arsenal.
PSG na Arsenal zitavaana Mei 30,2026, katika fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) itakayochezwa mjini Budapest, Hungary.
Neville ametupa karata yake kwa PSG, licha ya kwamba Arsenal imetoka kuandika historia ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya England (EPL), ambalo ni la kwanza kwao tangu mwaka 2004.
“Ni mechi ngumu sana kwao (Arsenal). Niwe mkweli tu, kwamba nafikiri PSG ni ‘levo’ nyingine kabisa. Wanaye Luis Enrique, ambaye ni kocha bora zaidi kwa sasa,” amesema Neville.
Arsenal wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu kwamba hiyo ni fainali yao ya pili kucheza kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika fainali yao ya kwanza mwaka 2006, waliukosa ubingwa baada ya kufungwa mabao 2-1 na Barcelona.


