12.9 C
New York

Igor Thiago: Kutoka maisha ya msoto hadi Kombe la Dunia 2026

Published:

LONDON, Uingereza

WAKATI kocha wa timu ya soka ya Taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti, alipotangaza kikosi kitakachokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu zitakazoanza Juni 11, 2026, uwepo wa jina la mshambuliaji wa Brentford, Igor Thiago, haukuwashangaza wengi kutokana na kiwango chake msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Kwa Igor, ni ndoto iliyotimia kwenda Kombe la Dunia, michuano itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico. Kwanini? Ni kutokana na aina ya maisha aliyopitia kabla ya ‘kutoboa’ kupitia mchezo wa soka.

BABA AIACHIA FAMILIA MAISHA YA MSOTO

Akiwa na umri wa miaka 13 tu mjini Gama, alipoteza baba. Hiyo ikaitumbisha familia kwa kiasi kikubwa, ikizingatiwa kuwa mama hakuwa akipata kipato kikubwa katika kazi yake ya kufanya usafi mitaani.

Kama mtoto wa kiume, licha ya umri wake mdogo, Igor alilazimika kuingia mitaani kutafuta kazi yoyote. Wakati mwingine, ungemkuta kwenye saiti za ujenzi wa majengo akiwa kibarua wa mafundi ili tu kupata pesa za kujikimu.

Kando na chagamoto hizo, bado Igor na kaka yake walijichanganya na wenzao wa mitaani kucheza ‘chandimu’, kabla ya kujiunga na U-17 ya klabu ya Vere akiwa na umri wa miaka 16.

Mwaka 2019, nyota njema ilionekana aliposajiliwa na Cruzeiro, ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ni ndoto yake kuja kuitumikia akiwa mchezaji wa soka la kulipwa.

Igor alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 2020. Alicheza mechi 64 na kufunga mabao 10 hadi alipoondoka klabuni hapo Machi, 2022.

ATUA ULAYA KWA MARA YA KWANZA

Aliiacha Cruzeiro baada ya klabu kongwe ya Bulgaria, Ludogorets Razgrad, kutangaza ofa nzuri. Katika msimu wake wa pili, alifunga mabao 20 katika mechi 53 za mashindano mbalimbali.

Hapo ndipo Club Brugge ya Ubelgiji ilimsajili kwa euro milioni 7.9 mwaka 2023. Kwa msimu mmoja pekee aliocheza soka la Ubelgiji, kabla ya kusajiliwa na Brentford mwaka 2024, Igor aliacha gumzo baada ya kupachika mabao 29.

AVUNJA REKODI EPL

Nyota huyo alitua Brentford kwa ada ya Pauni milioni 30 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyesajiliwa kwa fedha nyingi zaidi katika historia ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England (EPL).

Msimu wake wa kwanza England, 2024/25, haukuwa mzuri kwani alikosa mechi nyingi na kucheza nane tu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Safari hii, kwa maana ya 2025-26, mambo ni tofauti. Katika mechi 37 za EPL alizocheza, Igor ameweza kuingia kambani mara 22, akizidiwa na Erling Haaland tu katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Kwa upande wa timu ya Taifa, alianza kuitumikia Brazil mwanzoni mwa mwaka 2026 na kufunga bao lake la kwanza katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Croatia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Related articles

Recent articles