CATALUNYA, Hispania
USHINDI wa mabao 2-0 mbele ya Real Madrid jana Mei 10, 2026 umeipa Barcelona ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).
Barcelona wametwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi 14 dhidi ya Madrid inayoshika nafasi ya pili, pia ikiwa bado ina michezo mitatu mkononi.
Ifahamike kuwa El Clasico ya jana ni ya kwanza baada ya miaka 100 kuamua mbabe wa mbio za ubingwa wa La Liga.
Kwa upande mwingine, nyuma ya mafanikio hayo, yupo Hansi Flick na hilo ni taji lake la pili mfululizo kwa misimu miwili aliyokaa kwenye benchi la ufundi la Barcelona.
Chini ya Mjerumani huyo, msimu huu Barcelona wamemaliza mbio za ubingwa wakiwa wameshinda mechi zote 11 walizocheza hivi karibuni.
Kwa ujumla, Barcelona wamepoteza mechi nne pekee za La Liga msimu huu, wakishinda zote walizocheza katika uwanja wake wa nyumbani.
Ukiweka michuano mingine, Barca imeshinda mechi 42 kati ya 53 msimu huu, licha ya kuishia nusu fainali ya Copa del Rey na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Flick aliajiriwa Mei, 2024, wakati huo Madrid ikiwa bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa na La Liga, pia ikiongeza nguvu kwa usajili wa Kylian Mbappe.
Ndani ya misimu miwili ya Flick, Barca imeshatwaa mataji matano ya michuano ya ndani, wakati huu ukiwa ni msimu wa pili mfululizo kwa Madrid kuambulia patupu.


