BARCELONA, Hispania
FC Barcelona wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa La Liga baada ya kuichapa Real Madrid mabao 2-0 katika mchezo mkubwa wa El Clásico uliochezwa kwenye uwanja mpya wa Camp Nou.
Mshambuliaji Marcus Rashford alianza kuifungia Barcelona kwa mkwaju wa faulo uliovutia mashabiki wengi kabla ya Ferran Torres kuongeza bao la pili na kuthibitisha ushindi huo muhimu.
Kikosi cha kocha Hansi Flick kilihitaji sare pekee kutetea ubingwa huo, lakini kilionyesha ubora mkubwa kwa kuifunga Real Madrid mbele ya mashabiki wao na kuweka historia ya kutwaa taji hilo kupitia mchezo wa El Clásico kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Furaha katikati ya majonzi
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha wa Barcelona, Hansi Flick amesema: “Sitasahau siku hii kamwe. Imekuwa siku ngumu kwangu. Ilianza kwa kumpoteza baba yangu, lakini hapa timu yangu ni ya ajabu sana, ninaipenda, wako kama familia. Pia ninajivunia mashabiki wetu, hali ya uwanjani hapa ilikuwa ya kipekee, kushinda El Clásico ni jambo kubwa. Haikuwa rahisi,”.




