LONDON, Uingereza
KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amemuonya staa wake, Phil Foden, akimwambia hana uhakika wa kuitwa kwenye kikosi kitakachokwenda Kombe la Dunia.
Tuchel, kama ilivyo kwa makocha wote wa timu za taifa zilizofuzu fainali hizo za Juni-Julai, 2026, atawasilisha kikosi chake cha mwisho ifikapo Mei 30.
England imepangwa na Croatia, Ghana na Panama katika hatua ya makundi ya fainali hizo za FIFA.
Katika mechi zake mbili za kirafiki za hivi karibuni, England ilitoa sare ya bao 1-1 na Uruguay, kabla ya kutandikwa bao 1-0 na Japan.
Foden mwenye umri wa miaka 25, alitokea benchi katika mechi hizo lakini nyota huyo wa Manchester City hakuonesha kiwango kizuri.
Nyota huyo hajafunga bao katika mechi 22 alizoitumikia England hivi karibuni. Mara yake ya mwisho kufunga ilikuwa Oktoba, 2022.


