MERSEYSIDE, England
KINARA wa upachikaji mabao wa Sporting Lisbon ya Ureno, Luis Suarez Charris, ameingia kwenye rada za vigogo wa Ligi Kuu ya England, Liverpool.
Liverpool wanapitia kipindi kibaya baada ya hivi karibuni mshambuliaji wao, Mohamed Salah, kusema ataondoka mwishoni mwa msimu huu.
Sasa, kwa mujibu wa Gazeti la Correio da Manha la Ureno, macho ya mabosi wa Liverpool yametua kwa Suarez Charris.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa vigogo hao wa Anfield wamejadiliana na kufikia uamuzi wa kutenga Pauni milioni 70 za kumnasa straika huyo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, ameshafunga mabao 29 na kutoa ‘asisti’ tano katika mechi 35 za msimu huu.
Katika mechi 25 za Ligi Kuu (Primeira Liga), amefunga mara 24, huku michezo yake 10 ya Ligi ya Mabingwa ikizalisha mabao matano.
Hata hivyo, hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kusajili washambuliaji kutoka Ligi Kuu ya Ureno.


